Mkenda aagiza usimamizi tozo za ukaguzi bidhaa za mionzi

SERIKALI imeiagiza bodi mpya ya Tume ya Nguvu za Atomu (TAEC) isimamie tozo zinazokusanywa na tume hiyo katika ukaguzi wa bidhaa za mionzi.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameiagiza pia, TAEC itenge fedha kwa ajili ya kuwapa watumishi mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi.
Profesa Mkenda alitoa maagizo hayo Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi ya tume hiyo inayoongozwa na Profesa Joseph Msambichaka.
Alisema baadhi ya bidhaa zimekuwa zikifanyiwa ukaguzi usio wa lazima, jambo linalosababisha wafanyabiashara wengi kukwepa tozo hizo na kuleta vikwazo katika biashara.
Profesa Mkenda alisema TAEC imekuwa ikikusanya tozo kwa baadhi ya bidhaa ambazo hazina ulazima wa kukaguliwa ili kupata mapato, hivyo kufanya kazi nje ya malengo.
“Wakati nipo Wizara ya Kilimo, nilitembelea kiwanda cha kuchakata kahawa, mmiliki anasema ni rahisi kuuza kupitia Uganda kuliko Tanzania, nilipouliza shida ni nini, akasema matozo mengi, tozo mojawapo iliyotajwa ni ya tume, nilipokuja huku nilikutana nayo na tulipambana kuiondoa,” alisema Profesa Mkenda.
Aliongeza, “hatuwezi kufanya kazi kwa namna ambayo inasababisha mtu… anaona ni rahisi apeleke mzigo wake Uganda ambayo haina bandari, azungushe apeleke Mombasa kuliko kutoka Kagera kuleta Dar es Salaam. Kumbe ukikagua, kuna tozo usipokagua unapoteza kwa hiyo unakuta lengo la tozo linakuwa kubwa kuliko lengo la simamizi.”
Profesa Mkenda alisema baadhi ya bidhaa hutumia gharama kubwa katika ukaguzi ambazo ni thamani ya shehena na kusababisha wafanyabiashara kulipa tozo kubwa.
“Mzigo unapokaguliwa wanakutoza kama asilimia ya thamani ya shehena, sasa thamani ya shehena na gharama za ukaguzi vina uhusiano gani? Kwamba kama ni tani moja, kwa sababu huku kuna gharama kubwa zaidi, namna ya kupima unalipa hela nyingi zaidi kuliko tani moja ya kitu ambacho kina gharama ndogo kinachofanya tufanye hivi ni
tozo,” alisema.
Kuhusu mafunzo kwa watendaji, alisema kuna upungufu wa wataalamu wa masuala ya atomu na mionzi kwa kuwa wengi wamestaafu.
“Wakati jina linatafutwa la mtendaji mkuu tuligundua kuwa tumepungukiwa, kina Profesa Najat Mohamed
(Mkurugenzi Mkuu TAEC) wako wachache sana na waliosomea hivyo, wengine wameshastaafu kwa hiyo hatuna watu wengi na tunawahitaji huko vyuoni,” alisema.



