Wajasiriamali wanawake, vijana mipakani kuwezeshwa

SHIRIKA la Foundation For Civil Society (FCS) limeingia makubaliano ya miaka miwili na Benki ya Stanbic Tanzania kupitia mradi wa Stanbic Biashara Incubator unaolenga kuwainua wajasiriamali wanawake na vijana kwa kuwapatia ujuzi, maarifa, na fursa za ukuaji wa biashara maeneo ya mipakani.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam hii leo, Mkuu wa Kitengo cha Stanbic Biashara Incubator, Kai Mollel amesema kuwa lengo ni kuwawezesha wajasiriamali ili biashara zao ziweze kustawi na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa taifa.

“Tunatambua kuwa biashara ndogo na za kati (SMEs) ndizo zinazotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania. Zinatoa ajira kwa mamilioni ya watu na zina mchango mkubwa katika pato la taifa,”

“Hata hivyo, changamoto bado ni nyingi katika sekta hii, ikiwemo ukosefu wa elimu ya kifedha na mbinu bora za kusimamia biashara, changamoto za mitaji, na upatikanaji wa masoko,” amesema Mollel.

Ameongeza kuwa kwa wafanyabiashara wa mipakani, changamoto ni kubwa zaidi kutokana na vikwazo vya kisheria, ukosefu wa taarifa sahihi, na mazingira magumu ya kufanyia biashara, hali inayowafanya washindwe kufanikisha shughuli zao kwa urahisi na ufanisi.

“Benki ya Stanbic Tanzania inaamini kuwa Tanzania ni nyumbani kwetu, na hatuwezi kuwa na uchumi imara bila kuhakikisha biashara ndogo na za kati zinapata uwezeshaji wa kweli. Kupitia Biashara Incubator, tunajitolea kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao kwa viwango vya juu zaidi,” ameongeza Mollel.

Katika ushirikiano huu, wajasiriamali 250 wa mipakani na 100 wa Programu ya Ukuzaji wa Wasambazaji watapokea mafunzo maalum. Mafunzo haya yanajumuisha siku nane za stadi za uzabuni na mafunzo ya biashara yanayotolewa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ili kuwaandaa kushiriki kikamilifu kwenye minyororo ya thamani ya makampuni makubwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa FCS, Justice Rutenge, alisema kuwa mradi huu unafadhiliwa na TradeMark Africa (TMA) kwa msaada wa serikali za Uingereza kupitia FCDO, Ireland, na Norway.

Ametoa shukrani kwa wahisani hao kwa kuunga mkono juhudi za kuboresha biashara za mipakani na usimamizi wa haki za watumiaji.

“Tumejikita katika kuhakikisha sauti za wananchi zinasikika, na kwa kushirikiana na sekta ya umma na binafsi, tunawezesha wafanyabiashara kupata masoko.

Tunafurahia ubia wetu wa kihistoria na Stanbic ambao utasaidia kuvuna ujuzi wa wenzetu katika kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi,” amesema Rutenge.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button