Samia: Watatuheshimu
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Watanzania wakimaliza wenyewe changamoto zinazowakabili, mataifa mengine yatawaheshimu.
Ameyasema hayo Ikulu Dar es Salaam wakati akizindua Tume ya Rais ya Kutathmini kuhusu Masuala ya Mgogoro wa Ardhi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Rais Samia amesema kama Watanzania walivyotoa suluhu katika changamoto zingine kwenye taifa, suala la mgogoro wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kupitia tume zilizozinduliwa linaweza kupatiwa suluhisho.
“Sisi wenyewe kama Watanzania kama tulivyotoa suluhu za changamoto zingine zinazotuzonga kwenye taifa na hili nalo tutalipatia suluhisho na tukifanya hivyo, mataifa mengine yatatuheshimu sana,” alisema.
Alisema pia, inapotokea changamoto Watanzania wanapaswa kutumia akili zao wenyewe na kuhakikisha utatuzi wa changamoto hizo unapatikana kwa kushirikiana.
Rais Samia aliagiza tume hizo zifanye kazi kwa kujiamini, uadilifu na weledi wa hali ya juu kwa kuliweka taifa mbele.
“Sisi tuna imani kubwa na uwezo wenu, tunaamini mtatukwamua hapa tulipo na kama kawaida yetu, tutapata majibu ya changamoto zetu kwa kutumia maarifa yetu sisi wenyewe na hiyo ndiyo maana ya uhuru kwa Watanzania,” alisema.
Aliongeza: “Tume hizi tumezizindua na nadhani Katibu Mkuu Kiongozi ameshajitayarisha kamili kamili kwa tume hizi kuanza kazi, niwatakie kila la heri, kafanyeni kazi yenu kwa weledi na kwa maslahi mapana ya taifa”.
Uzinduzi wa tume hizo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais Samia, Desemba Mosi, mwaka jana mkoani Arusha
alipokukutana na kuzungumza na viongozi na wawakilishi wa wananchi wanaoshi eneo la Ngorongoro na maeneo
jirani.
Zitaongozwa na Jaji Gerald Ndika ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini kuhusu Masuala ya Mgogoro wa Ardhi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Musa Lyombe ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Tume hizo zinajumuisha uwakilishi wa wananchi wanaoishi katika eneo la Ngorongoro na zinatarajia kufanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu.



