BoT yaonya ulaghai upatu mtandaoni, 26 mbaroni
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema inaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya maofi sa wa Kampuni ya Leo Beneath London (LBL) wanaodaiwa kujihusisha na ulaghai ukiwamo wa kupokea amana, kutoa riba na kufanya uhaulishaji wa fedha bila kuwa na leseni.
Taarifa ya Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba imeeleza kuwa benki hiyo haijafanya mazungumzo wala kutoa maelekezo yoyote ya kupewa leseni au kuruhusiwa kwa kampuni hiyo tofauti na taarifa zinazosomeka mitandaoni.
Tutuba amehadharisha wananchi kujihusisha na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye anatoa huduma za kifedha bila kuwa na leseni ya benki kuu au wasimamizi wengine wa huduma za fedha.
“Benki Kuu inawaonya watu na taasisi ambazo zinatumia jina la Benki Kuu kuuhadaa umma katika vitendo vyao vya kihalifu, kuacha kufanya hivyo vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” ameeleza Tutuba.
Aidha, amewahimiza wananchi wanaotaka kupata huduma za kifedha watumie taasisi zenye leseni ambazo orodha yake inapatikana kwenye tovuti ya BoT au wasimamizi wengine wa sekta ya fedha nchini.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 26 wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya upatu mtandaoni bila kuwa na kibali cha BoT.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Mkurugenzi wa LBL, Najim Houmoud (34) mkazi wa Kigamboni, Hatibu Kudura (25) mkazi wa Kinondoni, Fatuma Hamisi (26) mkazi wa Kigamboni na Athumani Sadik (29) anayeishi Mabibo.
Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao walikamatwa kuanzia Februari 18 hadi 22, mwaka huu katika maeneo Mbagala, Gongolamboto, Tabata, Mbezi Magufuli, Ubungo Riverside na Mabibo.
Kamanda Muliro amesema Polisi kwa kushirikiana na BoT ilifanya uchunguzi wa LBL inayojihusisha na biashara ya upatu mtandaoni na kubaini haina uongozi maalumu.
Kadhalika, ilibaini uendeshaji wa biashara hiyo unahitaji wanachama kutoa kiasi cha fesha kuanzia Sh 50,000 ili kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama na kuchangisha fedha kwa kuwadanganya wananchi kwamba watapata faida kubwa huku wakidaiwa kushiriki kwenye shughuli za kampuni hiyo.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote kuacha kujihusisha na biashara za upatu mtandaoni bila kujiridhisha kwanza, kwa kuwa baadhi ya biashara hizo hazina leseni wala vibali kutoka kwa mamlaka za kisheria zinazohusika, hivyo kuhatarisha usalama wa fedha zao,” amesema Kamanda Muliro.



