Samia kuzindua ujenzi barabara Bagamoyo-Pangani-Tanga leo

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la mradi ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Mkange-Pangani-Tanga yenye urefu wa kilometa 256 ikijumuisha daraja la Pangani lenye urefu wa meta 525.

Anatarajiwa kuweka jiwe hilo ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tanga aliyoianza Februari 23, na leo ikiwa ni siku ya nne.

Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Aisha Malima alisema mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na serikali.

Malima aliieleza HabariLEO kuwa AfDB imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 169.98 sawa na Sh bilioni 390.1 na Serikali ya Tanzania imechangia Sh bilioni 58.47.

“Kazi zilianza Desemba 7, 2022 muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 36 ya ujenzi na miezi 36 ya kipindi cha uangalizi kwa upande wa daraja na miezi 12 kwa upande wa barabara,” alisema.

Katika ziara mkoani Tanga Rais Samia ametembelea wilaya za Handeni, Lushoto, Korogwe na Kilindi.

Akiwa huko ameahidi kuboresha zaidi miundombinu ikiwemo ya barabara ili kusaidia kufungua uchumi wa Tanga na kuwanufaisha wananchi.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button