Kambi uchunguzi wa afya Muhas kuwa endelevu

CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema kambi maalum ya huduma za afya inayotolewa bure kwa magonjwa yasiyoambukiza itakuwa endelevu ili kuenzi  mchango wa aliyekuwa mkuu wa chuo hicho na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.

Akizungumza leo Februari 26, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema programu hiyo wataisogeza maeneo ya kata na vijiji ili wananchi waweze wananchi wapate fursa ya kutambua afya zao.

Prof. Kamuhabwa amesema kuna magonjwa ambayo yanaweza kutibika na kuzuiliwa kwa kufuata mtindi mzuri wa chakula na kufanya mazoezi.

“Kambi hii ni maalum kuenzi mchango wa hayati Mwinyi katika sekta ya afya, wengi mnafahamu kwamba pamoja na uzee wake alipenda kufanya mazoezi, hivyo ni jukumu letu kuona tunatoa huduma bora za afya,” amesema Prof Kamuhabwa.

Aidha, amesema idadi ya watu waliojitokeza kufanya uchunguzi imeridhisha, hata hivyo amewataka wananchi kuwa mabalozi wa kuhamasisha wengine kujitokeza zaidi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kambi hiyo, Dk Ferdinand Machibya amesema leo wamejitokeza wananchi 130 na kwamba wanatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya 600 kwa siku mbili.

Dk Ferdinand amesema wananchi watakaobainika kuwa na magonjwa watashauriwa mahali sahihi kwa kupata huduma hizo.

Katika kambi hiyo, wananchi wanapata huduma za uchunguzi wa afya kwa magonjwa ya macho, masikio, pua na koo, kinywa na meno na magonjwa ya saratani ya matiti na shingo ya kizazi, homa ya ini na tezi dume kwa kipimo cha damu.

Mkazi wa Msakuzi, Dar es Salaam, Adela Bulusha ,86, ameshauri uwepo wa huduma za dawa katika kambi hizo ili kuwawezesha kukamilisha matibabu yao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button