Dira 2050 yataka jamii yenye ujuzi kukabili changamoto

RASIMU ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imesema ili kufi kia ukuaji endelevu wa kijamii na kiuchumi na kushindana kwa ufanisi kimataifa ifikapo 2050, Tanzania inatarajia kujenga jamii iliyoelimika vizuri, yenye ujuzi na inayobadilika.

Imebainisha kuwa inahitajika nguvu ya elimu katika kuongoza mabadiliko kwa kuwawezesha wananchi kupata maarifa muhimu, ujuzi na maadili ili kukabiliana na changamoto za maendeleo.

Inasema elimu ni msingi wa kukuza fikra makini, kutatua matatizo, ubunifu, uwezo wa uchambuzi, utaalamu katika nyanja mbalimbali na kukuza utamaduni wa kuendelea kujifunza.

Pia, rasimu hiyo inaeleza kuwa uwekezaji katika maendeleo ya watoto ni jambo lisiloepukika na husaidia kuweka msingi wa ujuzi wa utambuzi kihisia na kijamii katika kuandaa mazingira ya ujifunzaji endelevu na wenye mafanikio.

Inaeleza kuwa kwa kushughulikia mahitaji ya maendeleo, mtoto kutoka umri mdogo, hujenga nguvukazi imara, yenye ujuzi, hupunguza kukosekana kwa usawa na kuchangia katika ukuaji wa kijamii na kiuchumi.

Dira inaeleza kuwa programu za elimu bora kwa mtoto zinasaidia katika kukabiliana na umaskini, kukuza usawa wa kijinsia na kuwapa watoto stadi za awali za kusoma, kuhesabu na masuala ya kijamii kwa lengo la kujenga mafanikio ya kitaaluma na kiuchumi.

Pamoja na hayo, Dira inaeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika utoaji elimu na mafunzo ikichangiwa na uwekezaji mkubwa wa serikali katika miundombinu ya shule, mfano kufikia 2020, kiwango cha uandikishaji wa jumla kwa elimu ya msingi kilifikia asilimia 100 na 2023 kiwango cha mpito cha msingi hadi sekondari kilifikia asilimia 73.8, hivyo mfumo huo lazima uendelee kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya jamii ya ndani na ya kimataifa ifikapo 2050.

Inabainisha kuwa kuandaa vijana kwa uchumi wa dunia na mapinduzi ya viwanda kunahitaji kuweka kipaumbele katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati ili kuziba pengo lililopo na kutatua changamoto ya uwiano wa kijinsia, hasa katika masomo yaliyobainishwa hapo juu, kunahitajika kuendeleza na kukuza uwezo wa kuhimili mabadiliko, ujasiriamali, na elimu ya masuala ya kifedha.

Rasimu inaeleza kuwa stadi za maisha pia ni muhimu kwa ustawi katika ulimwengu wa mabadiliko hivyo kupitia njia hiyo, mfumo wa elimu wa Tanzania unaweza kukuza nguvukazi stahimilivu, imara, itakayoweza kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa sababu anzania inatarajia kuona mabadiliko makubwa ya fikra, watu wenye ujasiri, na uwezo.

Matarajio ya rasimu ya dira ya taifa 2050 ni kuwa na mfumo bora wa elimu na mafunzo jumuishi unaowajengea wahitimu maarifa na ujuzi, na wenye viwango vya vinavyotambulika kikanda na kimataifa.

Inatarajia kuona Tanzania inakuwa na mtoto aliyepata malezi na makuzi bora, mwenye stadi msingi za maisha na ujifunzaji endelevu. Pia, wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya jamii, wanaoajirika, na walio tayari kukabiliana na ushindani wa soko la ajira linalobadilika kutokana na mageuzi ya teknolojia.

Pia, inataja kuwa na jamii inayotumia maarifa na ujuzi na ubunifu kama msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kuwa na jamii inayojifunza bila kikomo kupitia mfumo endelevu wa elimu na mafunzo ili kujenga na kuimarisha maarifa na ujuzi wa hali ya juu kwa ajili ya kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo endelevu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button