Viwanda kinara miradi mingi TIC minne ya Samia

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema sekta ya viwanda imeongoza kusajili miradi mingi katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ikifuatiwa na sekta ya usafirishaji.

Mkurugenzi Mkuu wa TIC, Gilead Teri alisema hayo Dodoma jana akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya kituo hicho katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Teri aliwaeleza waandishi wa habari kuwa takribani viwanda 917 vilisajiliwa TIC katika kipindi cha mwaka 2021-2024 ambayo ni sawa na asilimia 50 ya miradi yote iliyosajiliwa na TIC katika kipindi hicho huku viwanda 390 vikisajiliwa 2024.

“Viwanda 390 katika siku 360 za mwaka tulikuwa na wastani wa kuanzishwa kiwanda kimoja kila siku katika nchi yetu, mkipita huku njia ya Kibaha Zegereni mpaka Mlandizi mkiingia ndani kuna idadi ya viwanda ambavyo hamtaamini,” alisema Teri.

Teri alisema sekta iliyofuatia kwa kusajili miradi mingi katika kipindi hicho ni sekta ya usafirishaji iliyosajili asilimia 19 ya miradi yote.

Alisema miradi mingi imesajiliwa kutokana na diplomasia ya uchumi iliyochangiwa na ziara za kimkakati za Rais Samia Suluhu Hassan katika mataifa ya nje ambazo zimechangia kusainiwa kwa makubaliano kadhaa kati ya TIC na jumuiya za uwekezaji.

Kwa upande wa sekta ya usafirishaji, Teri alisema miradi mingi imesajiliwa kutokana na kuongezeka kwa ufanisi katika huduma za bandari na vivutio vinavyotolewa na TIC kwa wafanyabiashara na wawekezaji waliosajiliwa na kituo hicho.

“Ukiagiza vichwa viwili vya lori ule msamaha wa ushuru wa kuingiza kichwa hicho unaoupata unaweza kuongeza nusu na ukaagiza kichwa cha tatu, ni sekta ambayo Watanzania wengi sana wameongezeka katika miaka minne iliyopita hasa kupeleka mizigo nchi jirani,” alisema Teri.

Alitaja sekta zingine zilizoongezeka kukua na kusajili miradi mingi ni majengo ya biashara asilimia 11.2, utalii asilimia 10.5 na kilimo asilimia 9.9.

Aidha, Teri alisema katika kipindi hicho cha uongozi wa Rais Samia, TIC imevunja rekodi ya kusajili miradi na mitaji mikubwa ikifananishwa na miaka mingine.

“Kumekuwa na ingezeko kubwa la wastani wa uwekezaji nchini 2021 ilisajiliwa miradi 256, mwaka 2022 miradi 293, mwaka 2023 miradi 526 na mwaka jana tulisajili miradi 901 ambayo ni rekodi haijawahi kutokea tangu kuanzishwa TIC,” alisema.

Aliongeza: “Pia mitaji iliyoingia nchini iliongezeka 2021 ilikuwa Shilingi bilioni 3.7, mwaka 2022 bilioni 4.5, mwaka 2023 bilioni 5.7, mwaka 2024 bilioni 9.3 mwaka huu tumelenga miradi 1,500 na mitaji Dola za Marekani bilioni 15”.

Teri alisema katika miaka minne iliyopita wawekezaji mahiri na wawekezaji wa ndani wameongezeka na wapo kwenye sekta ya viwanda, mashamba na kongani.

Alisema kuanzia Januari 2021 hadi Januari mwaka huu, Watanzania wanamiliki asilimia 34.3 katika miradi iliyosajiliwa na asilimia 42.6 inamilikiwa na wageni.

“Juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kushusha kiwango cha chini cha kuruhusu kusajili mradi TIC ili kupata vivutio kutoka dola za Marekani 100,000 mpaka dola 50,000 kimesaidia kuongeza usajili wa miradi ya wawekezaji wa ndani,” alibainisha Teri.

Aidha, katika kipindi cha kuanzia Januari 2021 hadi Januari 2025, TIC imesajili miradi 2,020 ambayo ni ongezeko la asilimia 91 ikilinganishwa na miradi 1,057 iliyosajiliwa katika kipindi cha 2017 hadi 2020.

“Thamani ya mitaji ya miradi hii inakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 23.67, ikiongezeka kwa asilimia 188.7 kutoka Dola za Marekani bilioni 8.2 katika kipindi cha 2017-2020,” alieleza.

Alisema kumekuwa na ongezeko la asilimia 284.5 kutoka ajira 136,232 zilizozalishwa kipindi cha miaka minne ya kuanzia mwaka 2017 mpaka 2020, mpaka ajira 523,891 zinazotarajiwa kuzalishwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2021-2024.

“Lakini pia thamani ya mitaji ya miradi iliyosajiliwa imepanda kwa asilimia 188.7 kutoka Dola za Marekani bilioni 8.2 hadi bilioni 23.67, ishara ya kuongezeka kwa uaminifu wa wawekezaji kwa Serikali ya Awamu ya Sita,” alisema Teri.

 

Imeandikwa na Zena Chande na Ally Ruambo

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button