Samia: Maboresho Bandari ya Tanga kuongeza ufanisi, tija

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa maboresho ya Bandari ya Tanga ambayo yamegharimu shilingi bilioni 429 yatakwenda kuongeza ufanisi mkubwa wa bandari hiyo pamoja na kuliongezea tija taifa.
Ameyasema leo Machi 01 wakati akizungumza na wafanyakazi wa Bandari ya Tanga alipotembelea bandari hiyo kwa ajili ya kukagua maboresho ya mradi wa gati mbili mpya katika bandari hiyo.
Rais Samia ameeleza kuwa baada ya maboresho hayo mpaka sasa bandari hiyo imehudumia tani milioni 1.2 ikiwa ni ongezeko ya zaidi ya tani laki 7 ukilinganisha na mwaka 2019/20.
Ameeleza faida nyingine ya maboresho hayo kuwa yataisaidia serikali kupata fedha zaidi zitakawezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuleta ajira kwa wakazi wa Tanga ambapo maboresho hayo yameongeza ajira kutoka 6000 hadi elfu-17.
Hata hivyo Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa amesema ili kufungua mkoa wa Tanga kiuchumi wanatarajia kupeleka miradi yenye thamani ya shilingi trilioni 1.1 kwa mwaka wa fedha 2025/26.



