Samia: Tanzania imefunguka, ni salama kwa uwekezaji
Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wawekezaji kuwa “Tanzania imefunguka kwa uwekezaji, Tanzania ni salama kwa uwekezaji, na sera za uwekezaji za Tanzania ni rafiki na endelevu.”
Aidha, Rais Samia amesema kuwa Serikali inazidi kuwakaribisha wawekezaji na kuwa itaendelea kuweka sera rafiki, zinazotabirika na zinazowazesha wawekezaji nchini kuwa washindani katika soko la ndani na soko la kimataifa.
Ameyasema hayo leo Machi 01 wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa Ujenzi wa Kala wa kuhifadhia gesi ya LPG ya GBP Tanzania katika Jiji la Tanga.
Taarifa ya Ikulu imesema uwekezaji huo unaogharimu dola za marekani milioni 50 unaendana na lengo la Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia la kuimarisha upatikanaji wa gesi ya kupikia.
Amesema kuwasikia na kuwaona wawekezaji mbalimbali ikiwemo kampuni ya GBP wakieleza kuwa wananufaika na mazingira bora ya uwekezaji nchini ni kielelezo kuwa sera za biashara na uwekezaji zinaleta matokeo yanayokusudiwa.
Katika hatua nyingine Rais Samia amefanya ziara katika Bandari ya Tanga kujionea maboresho yaliyofanywa na Serikali kupitia uwekezaji wa Shilingi Bilioni 429 uliomarisha uwezo na ufanisi wa bandari hiyo.
Akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Samia amesema kuwa maboresho yanayofanywa na Serikali katika Bandari Kuu kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi, yaani Dar es Salaam, Mtwara na Tanga kwa sasa na Bagamoyo kwa siku zijazo, yanaenda kuihakikishia Tanzania nafasi yake kama lango kuu la kuingia Afrika Mashariki na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara, viwanda na uwekezaji.
Akizungumzia uimarishaji wa miundombinu katika Mkoa wa Tanga, Rais Samia amesema kuwa Serikali imepanga kujenga Barabara ya Handeni-Kiberashi-Kijungu hadi Singida kwa utaratibu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Mkuu huyo wa nchi amesema barabara hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya Bandari ya Tanga, na Serikali itamtafuta mwekezaji atakayejenga barabara hiyo kwa fedha zake mwenyewe na kisha watumiaji ikiwemo malori ya mizigo kulipia matumizi ya barabara hiyo inayofupisha safari.
Leo Rais Samia amehitimisha ziara yake ya siku 7 mkoani Tanga akifika Wilaya zote nane za Mkoa huo ambapo alizungumza na wananchi na kutembelea miradi ya maendeleo ya Serikali yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 600 na miradi ya sekta binafsi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 500.



