Rais Samia atoa msimamo bandari

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka watumishi wa bandari nchini kuwa tayari kufanya kazi kwa bidii, uadilifu kuendana na teknolojia mpya inayokuja kutokana na maboresho ya bandari yanayoendelea, kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuchochea maendeleo.

Rais aliyasema hayo jana mjini Tanga alipotembelea Bandari ya Tanga na kuzungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo.

“Wenzenu huko nje wanasema ‘Mama mimi naomba kazi, lakini naomba nipange bandari.’ Kuna nini? Sijui kwa nini kila mtu anataka kuja bandari lakini kwa hivi karibuni imepungua kidogo, hasa baada ya kuingiza sekta binafsi bandarini. Lakini kule nyuma kila mmoja alitaka bandari, kuna nini? Mimi sijui, lakini nanong’onezwa kilichopo,” alisema Rais Samia.

Aliagiza Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kusimamia uwajibikaji wa watumishi na kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara watakaofanya vitendo vya kuhujumu mamlaka hiyo.

“Naridhishwa na maboresho katika bandari zetu. Kipindi cha nyuma hali ilikuwa mbaya sana. Nilikuwa najiuliza, Bodi nzima inasimamia kumtetea mhujumu na wanajua wanachokifanya, lakini sasa hivi hali imebadilika. Hakikisheni vitendo vya kuhujumu uchumi ndani ya bandari zetu vinaepukwa,” aliongeza.

Aidha, aliagiza Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kutafuta mwekezaji atakayejenga barabara ya Handeni – Singida yenye urefu wa kilometa 340 ambayo gharama za ujenzi zitarejeshwa kupitia tozo za barabara.

“Barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo yetu ya bandari, nimezungumza na Waziri hii barabara tuifanye kwenye PPP, tusiwaachie Wizara ya Ujenzi hii barabara haitakwenda haraka,” alisema Rais Samia.

Alieleza kuwa barabara hiyo ni muhimu kwani ndiyo inayotarajiwa kubeba magari makubwa ya mizigo yanayotoka Tanga na kupeleka maeneo mengine na hivyo kuagiza iwekewe mageti ‘road tolls’ kwa ajili ya watu kulipa.

“Najua kuna watu wanalalamika huko huyu rais vipi analipisha watu kupita kwenye barabara, ninafahamu ninachofanya. Lipisheni kupitisha mizigo watakaopita binafsi walipe,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameeleza kuwa barabara ya Handeni – Kiberashi hadi Singida ikijengwa italeta ufanisi mkubwa wa Bandari ya Tanga kwani itapunguza usafiri wa kwenda Singida kwa takribani kilometa 250 na kupunguza matumizi ya mafuta kati ya lita 100 mpaka 120.

Akizungumzia maboresho ya bandari katika ukanda wa Bahari ya Hindi alisema yataongeza ufanisi wa bandari hizo na mapato ya serikali, pamoja na kufungua fursa za uwekezaji wa kiuchumi.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua maboresho ya gati mbili mpya katika Bandari ya Tanga, alisema maboresho hayo yanawanufaisha wananchi kwa fursa za ajira na wafanyabiashara wataweza kupokea na kusafirisha mizigo kwa gharama nafuu.

Akitolea mfano wa Bandari ya Tanga, ambayo imeboreshwa kwa gharama ya Sh bilioni 429, Rais alisema bandari hiyo imeongeza ufanisi na kuliongezea taifa tija.

Alisema hadi sasa, imehudumia tani milioni 1.2, ongezeko la zaidi ya tani 700,000 ikilinganishwa na mwaka 2019/20.

Profesa Mbarawa alisema wizara yake iko kwenye mazungumzo ya kutafuta mwekezaji wa kujenga barabara ya Handeni -Singida kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Tanga.

Pia, alisema maboresho hayo yameongeza ajira kutoka 6,000 hadi 17,000 huku mapato yanayotokana na bandari yakitarajiwa kusaidia miradi ya maendeleo na kuinua uchumi wa nchi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button