Barabara ya Handeni-Singida kujengwa kwa PPP

RAIS Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara ya Ujenzi kukaa na Wizara ya Uchukuzi kukubaliana kwa pamoja kutafuta mwekezaji atakayeshirikiana nao kujenga barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Chemba – Kwamtoro – Singida (km 340) kwa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Rais Samia alieleza hayo jana alipotembelea Bandari ya Tanga na kuzungumza na wafanyakazi wa Bandari mkoani Tanga na kusisitiza umuhimu wa barabara hiyo katika kurahisisha usafiri na kuchochea uwekezaji kati ya Mkoa wa Tanga na Singida.
“Barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo yetu ya bandari, nimezungumza na Waziri hii barabara tuifanye kwenye PPP, tusiwaachie Wizara ya Ujenzi hii barabara haitakwenda haraka,” amesema Rais Samia.
Alisema barabara hiyo ni muhimu kwani ndiyo inayotarajiwa kubeba magari makubwa ya mizigo yanayotoka Tanga na kupeleka maeneo mengine na hivyo kuagiza iwekewe mageti kwa ajili ya watu kulipa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alieleza kuwa barabara ya Handeni – Kiberashi hadi Singida ikijengwa italeta ufanisi mkubwa wa Bandari ya Tanga kwani itapunguza usafiri wa kwenda Singida kwa takribani kilometa 250 na kupunguza matumizi ya mafuta kati ya lita 100 mpaka 120.



