Samia: Tanzania imefunguka kwa uwekezaji

RAIS Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania imefunguka kwa uwekezaji na ni nchi salama yenye sera za uwekezaji rafiki, endelevu na zinazotabirika hivyo amewataka waendelee kuja kuwekeza.
Aidha, ametaka sheria na kanuni za mafuta zibainishe wazi kuhusu Bandari ya Tanga kuwa ni eneo linalohudumia wafanyabiashara wa mafuta kutoka Ukanda wa Kaskazini, hivyo wanunulie mafuta hayo huko ili kupunguza msongamano wa malori katika Bandari ya Dar es Salaam.
Aliyasema hayo jana jijini Tanga wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia gesi ya LPG ya Kampuni ya mafuta ya GBP Tanzania, uwekezaji unaogharimu Dola za Marekani milioni 50.
“Niwapongeze sana kwa uwekezaji huu wa Dola milioni 50 si mdogo ni mradi unaokwenda kuunga mkono ajenda yangu ya nishati safi ya kupikia,” alisema Rais Samia.
Alisema mradi huo na mingine pamoja na taarifa iliyotolewa kwake kuhusu mradi huo na Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Mafuta wa Kampuni ya GBP-Tanzania Ltd, Badal Soud ya kwamba nchi imepiga hatua ya maendeleo na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, ni ishara kuwa sera zilizowekwa za uwekezaji zinaleta tija.
“Niwahakikishie wawekezaji wote na GBP kuwa, Tanzania imefunguka kwa uwekezaji, Tanzania ni salama kwa uwekezaji na ahadi yetu ni kuendelea kuwa na sera za uwekezaji rafiki, endelevu na zinazotabirika, niwakaribishe waje kuwekeza kwa sababu na masoko yapo,” alisema Rais Samia.
Alimshukuru mwekezaji huyo kwa mrejesho alioutoa kuhusu sera za uwekezaji kuwa rafiki na kusema wanaposema wenyewe wawekezaji inatoa taswira halisi ya ukweli wa jambo hilo na kwamba serikali itaendelea kuziboresha ili kuwa na tija zaidi.
Akizungumzia mradi huo wa ghala la gesi ya LPG, Rais Samia alisema ni mradi utakaochochea upatikanaji wa nishati safi ya kupikia hivyo kumsaidia kuendeleza ajenda yake ya nishati safi Afrika.
Alisema mradi huo utakapokamilika utasaidia wananchi wengi kupata nishati safi na kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambazo si safi.
Aidha, alisema kampuni hiyo ina dhamira ya kuwekeza kwenye vituo vya kujaza gesi kila mkoa nchini na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono huku akiwaomba wakamilishe mradi huo mapema ili zile ajira zaidi ya 2,000 alizozitaja mkurugenzi wa kampuni hiyo zianze kutolewa kwa wananchi.
Mbali na hayo, aliipongeza kampuni hiyo kwa kutimiza miaka 25 tangu kuanza huduma nchini na kusema imepitia mazuri na changamoto ila kwa ustahimilivu wake imetimiza miaka hiyo kwa mafanikio makubwa.
Kuhusu kampuni hiyo kupewa idhini na serikali ya kuleta mafuta na kuhifadhi katika bandari ya Tanga kwa ajili ya usambazaji wa Kanda ya Kaskazini, Rais Samia alisema inafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na serikali lakini bado wafanyabiashara wa mikoa ya Kaskazini wanaenda kuchukua mafuta bandari ya Dar es Salaam.
“GBP wanafanya kazi nzuri ila wale wanaosambaza bado wanachukulia mafuta Bandari ya Dar es Salaam, wakati akiba iko Tanga, nilishatoa maagizo ila naona hayajatekelezwa, sasa kama ni sheria au kanuni haziko sawa ziwekwe sawa iwe sheria, wachukulia mafuta hapa (Tanga),” alisema.
Jana, Rais Samia alihitimisha ziara yake ya siku saba mkoani Tanga kwa kutembelea wilaya zote nane za mkoa huo na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo sambamba na kutembelea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.



