Umuhimu wa mawasiliano katika kukuza uchumi

MAWASILIANO ni nyenzo muhimu kwa nchi yoyote ile duniani.

Kwa nchi yenye watu wenye kipato cha kati na maskini kama Tanzania mawasiliano huwa muhimu zaidi katika kukuza uchumi.

Hii ni kwa sababu mawasiliano ni muhimu zaidi katika kuiwezesha familia, kaya, mtaa, kitongoji, kijiji hadi taifa kukuza uchumi kupitia shughuli mbalimbali ambazo pengine bila mawasiliano isingewezekana kuzitekeleza kwa namna yoyote.

Kwa mujibu wa wataalamu, mawasiliano hurahisisha biashara, mazingira ya uwekezaji na usambazaji wa taarifa na
hivyo kuruhusu Kampuni, watu binafsi na sekta mbalimbali kufanya kazi kwa urahisi na ufanisi.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mwesiga Felician, alipozungumza kwenye semina ya wahariri, wandishi wa habari na watangazaji wa vyombo vya habari mkoani Mwanza.

Anasema mawasiliano huimarisha umoja, amani na mshikamano wa taifa kwa kuwezesha watu kuelewana na kushirikiana na kupitia mawasiliano, jamii zinaweza kushughulikia changamoto zao kwa pamoja, kueneza ujumbe wa amani na kuepuka migogoro pia.

Anaongeza kwamba viongozi wa serikali na wadau wengine wanaweza pia kutumia mawasiliano kufikia wananchi ili kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa.

Aidha, anasema mataifa yanatumia mawasiliano rasmi kama ya kidiplomasia na mikutano ya kimataifa kubadilishana mawazo, teknolojia na rasilimali hali inayo ongeza maelewano baina ya mataifa, kuimarisha biashara kimataifa na kuweka maendeleo ya pamoja.

Felician anasema mawasiliano ni mhimili wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa na bila mawasiliano madhubuti, taifa haliwezi kufanikisha maendeleo endelevu na uhusiano imara wa kimataifa.

Kwa kuzingatia umuhimu huo, Felician anasema serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ifanye mapinduzi makubwa ya kupigiwa mfano katika sekta ya mawasiliano kutokana na kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.

Takwimu za Sekta
Felician anasema Tanzania imepata mafanikio makubwa kwenye sekta ya mawasiliano na kwamba kwa mujibu wa Ripoti ya Sekta ya Mawasiliano ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 inayoishia Desemba 2024, jumla ya laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 80.7 katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba, 2024 hadi milioni 86.8 kwa robo ya mwaka inayoishia Disemba 2024 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 7.7.

Akielezea mchanganuo ya idadi za laini za simu za mkononi (P2P) na mezani, anasema laini za simu za mkononi na
mezani zilizosajiliwa kwa ajili ya mawasiliano ya binadamu zimeongezeka kwa takribani milioni 7.8 katika robo mwaka inayoishia Desemba 2024.

Laini za simu kimkoa
Alisema idadi ya laini za simu kwa kila mkoa inaonesha kuwa katika robo ya pili ya mwaka 2024/2025, mkoa wa
Dar es Salaam ulishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na laini milioni 15.98, ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza laini milioni 5.75, Arusha laini milioni 5.23, Mbeya laini milioni 4.99 na Dodoma ilishika nafasi ya tano kwa kuwa na laini milioni 4.64 Feliciana anasema kwenye matumizi ya matumizi ya intaneti asilimia 91 ya Watanzania wamefikiwa na huduma ya kasi ya intanenti ya 3G na asilimia 88 (4G) huku asilimia 20 wakiwa wamefikiwa na matumizi ya 5G.

Anaeleza kuwa kwa sasa watu milioni 23 wanamiliki simu janja. Anasema takribani dakika bilioni 42.5 zilitumika katika robo mwaka iliyoishia Desemba 2024 ikilinganishwa na dakika bilioni 41.1 katika robo mwaka iliyoishia Septemba 2024.

Anasema katika kipindi hicho, idadi ya dakika nje ya mtandao ilikuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na ndani ya
mtandao katika robo ya mwaka iliyoishia Desemba 2024. “Sekta ya mawasiliano ni sekta wezeshi kwa sekta  zingine za kiuchumi,” anasema na kuwataka wanahabari kuhakikisha wanaandika kwa kina kuhusu umuhimu na faida za sekta za mawasiliano katika kukuza uchumi wa nchi.

Meneja wa TCRA kanda ya ziwa Mhandisi Imelda Banali anasema lengo la TCRA kutoa semina hiyo kwa waandishi wa habari ni kuwajengea uwezo wa namna ya kuandika na kuchambua repoti na takwimu mbalimbali zinatolewa na
mamlaka ili waiwezeshe jamii kuwa na uelewa mpana wa shughuli zinazofanywa na TCRA.

“Nia yetu hasa ni kupata wandishi wabobezi kutoka mikoa ya kanda ya ziwa watakaokuwa wabobezi wenye weledi na uelewa katika kuandika habari za sekta ya mawasiliano,” anasema. Anasema vyombo vya habari vina nafasi kubwa sana ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu na faida za sekta ya mawasiliano nchini katika kukuza uchumi.

“Tumieni vyombo vyenu na nafasi zenu katika kupeleka elimu hii kwa watu, ili waweze kuifahamu vizuri sekta ya mawasiliano, iweze kuwanufaisha kiuchumi,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button