Tanzania yanga’ara uwekezaji kutoka nje

UWEKEZAJI wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) umeendelea kuongezeka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, imefahamika.
Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2024 kuhusu uwekezaji wa mitaji binafsi kutoka nje inaonesha mwaka 2023 uwekezaji wa mitaji binafsi kutoka nje uliongezeka kwa asilimia 3.9 na kufikia Dola za Marekani milioni 23,042.5.
“Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na ongezeko la asilimia 5.8 la uwekezaji wa moja kwa moja (FDI), hususani kutoka kwenye faida zilizorudishwa pamoja na mikopo kutoka kwa wanahisa wakubwa,” imeeleza ripoti hiyo iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Imeongeza: “Matokeo haya yanaashiria imani waliyonayo wawekezaji juu ya uimara wa uchumi wetu kutokana na mazingira bora ya biashara na uwekezaji”.
Ripoti hiyo imeandaliwa kwa ushirikiano wa taasisi tatu ambazo ni BoT, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Imetaja nchi zilizoongoza kwa uwekezaji wa moja kwa moja ni Mauritius, Australia, Uingereza, Barbados, Uholanzi na Afrika Kusini.
“Kwa upande wa limbikizo, orodha ya nchi 10 kwa ukubwa wa uwekezaji zilibaki takribani zilezile huku Uingereza ikiendelea kuongoza kwa Dola za Marekani milioni 5,152.6 mwaka 2023.
Nchi nyingine zilizokuwa na uwekezaji mkubwa ni pamoja na Norway, Mauritius na Uholanzi,” imeeleza ripoti.
Imeeleza mwaka 2023 uwekezaji wa moja kwa moja uliongezeka kwa asilimia 14.7 na kufikia Dola za Marekani
milioni 1,648.9 ikilinganishwa na mwaka 2022.
“Ukuaji huu ulitokana hasa na ongezeko kubwa la mikopo kutoka kwa wanahisa, ambapo mchango wake kwenye jumla ya mitaji ya moja kwa moja uliongezeka hadi asilimia 43.1 kutoka asilimia 8.7 mwaka uliopita,” imeeleza ripoti.
Imeongeza: “Ongezeko hili linaonesha juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji,
sambamba na mageuzi ya kimuundo na uendelezaji wa huduma za kidijiti katika sekta mbalimbali”.
Ripoti imeeleza kuwa mwaka 2023 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ulifanyika zaidi kupitia mikopo ya muda mrefu na faida zilizorejeshwa kutoka kwenye uwekezaji.
Pia, imeeleza kulikuwa na mabadiliko ya vyanzo vya mitaji kutoka kwenye uwekezaji wa wanahisa na urejeshwaji
wa faida kwenda kwenye mikopo ya muda mrefu kutoka kwa wanahisa.
“Mabadiliko haya ni kielelezo wawekezaji wana imani na ukuaji wa uchumi, sambamba na jitihada za uboreshaji mazingira ya uwekezaji,” imeeleza.
Ripoti imeeleza mwaka 2023 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ulijikita zaidi katika shughuli za uchimbaji madini na uchorongaji, uzalishaji bidhaa viwandani, fedha na bima, pamoja na habari na mawasiliano na kwa pamoja zilichangia asilimia 82.4 ya jumla ya uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.
“Shughuli hizi zilikuwa miongoni mwa shughuli tano za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi zaidi katika mwaka 2023, isipokuwa shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani,” ilisema.
“Uwekezaji katika shughuli za habari na mawasiliano uliongezeka zaidi ya mara mbili hadi Dola za Marekani milioni 198, ukichochewa na mahitaji makubwa ya huduma za mtandao na miamala ya pesa kupitia simu za kiganjani,” imeeleza.
Ripoti imeeleza uwekezaji wa mitaji katika shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani uliongezeka zaidi ya mara
mbili hadi kufikia Dola milioni 361 mwaka 2023.



