Benki ya Dunia yasifu sera za Rais Samia

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dk Zarau Kibwe amepongeza uongozi na sera za kiuchumi za Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk Kibwe amesema Tanzania iliwekewa ukomo wa kiasi cha Dola bilioni tano za Marekani (zaidi ya Shilingi trilioni 10) kabla ya Rais Samia lakini sasa kiwango hicho kimefikia Dola bilioni 12 (zaidi ya Shilingi trilioni 25).

Alisema hayo wakati akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyemtembelea ofisini kwake jijini Washington nchini Marekani, ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini humo.

“Sijui huko nyumbani kama mnaliona au kulizungumza hili. Katika muda mfupi ambao, Rais Samia ameingia madarakani, ukomo wa Tanzania kwenye uhusiano wake na Benki ya Dunia umeongezeka kutoka Dola bilioni tano hadi bilioni 12. Hili si jambo la kawaida,” alisema Dk Kibwe.

Aliongeza: “Lakini suala hapa si fedha pekee. Kuongezeka huku kwa hadhi na kuaminika kwa nchi kumeipa pia, mwonekano wa tofauti katika uga wa kimataifa. Hivi sasa Tanzania inatazamwa kama moja ya mataifa yanayoendeshwa vizuri barani Afrika”.

Dk Kibwe ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika inayohusisha takribani nchi 23.

Mtanzania wa kwanza alikuwa, Christopher Kahangi aliyeshika wadhifa huo kati ya mwaka 1968 hadi mwaka 1970.

Ulega alimweleza, Dk Kibwe kuwa Watanzania wanaona fahari kuwa na mwenzao aliyeshika wadhifa huo.

Alimweleza maendeleo ya miradi kadhaa ya ujenzi wa barabara, mwendokasi na madaraja ambayo taasisi hiyo imetoa mikopo ili iendelezwe.

Ulega alimueleza Kibwe kuhusu tatizo la baadhi ya wakandarasi kutoka nchi za nje waliopewa kazi ya kujenga Tanzania lakini miradi haikamiliki kwa wakati kwa sababu malipo yao hufanywa kwenye nchi zao ambako ndiko wana akaunti.

“Sasa ninyi ndiyo mnaowalipa. Sisi tunaona ni vema hizi kampuni ziambiwe zilipe haraka ili kazi ziendelee au
wafungue akaunti zao Tanzania ili iwe rahisi kwao kulipa na mambo yasilale,” alisema.

Dk Kibwe alimweleza, Ulega kwamba wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Masuala ya Nishati uliofanyika Dar es
Salaam alishuhudia mabadiliko makubwa kwenye ujenzi wa barabara za mijini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button