Tril 67/- zawekezwa miradi miaka minne

SERIKALI imesema Sh trilioni 67 zimewekezwa kwa miaka minne katika miradi ya uwekezaji nchini.
Aidha, katika kipindi hicho cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tangu 2021, miradi 2,099 imesajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) huku miradi 1,982 ikianzishwa.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hayo alipofanya ziara katika bandari kavu ya Kwala na eneo la viwanda la Sino Tan Vigwaza, Kibaha mkoani Pwani jana.
Msigwa alisema tangu Machi 2021 mpaka Februari 2025, miradi ya uwekezaji na mitaji ikiwemo uwekezaji katika sekta ya viwanda imekuwa na ongezeko kubwa.
“Uwekezaji katika viwanda ni sehemu muhimu na kubwa iliyoleta matokeo chanya katika kampeni ya nchi yetu ya kuleta mageuzi ya kiuchumi,” alisema.
Aliongeza: “Utaona katika miradi iliyoanzishwa, miradi ya ubia imefikia 476, miradi iliyohusisha upanuzi wa maeneo ya uwekezaji ni 117, miradi ya Watanzania ni 719 na miradi ya wageni ni 904.”
Msigwa alisema sekta ya viwanda ndiyo inayoongoza kwa uwekezaji nchini na kwa kuanzia 2021 hadi Februari mwaka huu, miradi ya viwanda 951 imesajiliwa.
“Miradi hii inatarajiwa kuleta ajira 124,339 na kuwekeza mitaji ya takribani Sh trilioni 27, miradi hii ya viwanda inachukua asilimia 45 ya miradi ya sekta zote iliyosajiliwa katika mwaka 2021 hadi 2025,” alisema.
Kwa upande wa mitaji, Msigwa alisema miradi ya viwanda imechukua asilimia 42 ya mitaji ya sekta zote iliyosajiliwa katika kipindi hicho na kufanya miradi ya viwanda kuwa ndiyo sekta inayoongoza sekta zote kwa idadi ya miradi, mitaji na ajira.
“Jumla ya miradi 951 ya viwandani imesajiliwa, miradi mipya ya viwandani 917 imeanzishwa, miradi 36 imehusu upanuzi wa viwanda, miradi 244 ya viwanda ni ya Watanzania, imesajiliwa, miradi ya viwandani ya wageni 501 imesajiliwa, miradi ya ubia 206,” alisema.
Msigwa alisema mchanganuo unaonesha katika miradi hiyo ajira za viwandani ni 124,339.
“Jambo kubwa na zuri ni kwamba takwimu zinatuonesha idadi ya viwanda imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa mwaka hadi mwaka, jambo ambalo linathibitisha kuwa safari ya Tanzania ya viwanda inakwenda vizuri na hatua ambazo serikali yetu ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inakwenda vizuri na kwa mafanikio makubwa,” alisema.
Alisema Mkoa wa Pwani unashika nafasi ya pili katika kuvutia uwekezaji nchini ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam.
Msigwa alisema kuanzia 2021 hadi Februari 2025, Mkoa wa Pwani umepokea miradi ya uwekezaji 369 na asilimia 67 ya miradi hiyo ni viwanda ambavyo jumla yake imefikia 247.
“Aidha, mitaji iliyowekezwa na sekta zote kwa mkoa wa Pwani ni Sh trilioni 12.4, asilimia 61 ya mitaji hiyo inatokana na sekta ya viwanda ikiwa na mitaji ya Sh trilioni 7.5,” alisema.



