INEC yapewa ushauri kugawa majimbo

WADAU wa masuala ya siasa wameshauri mchakato wa kugawa majimbo uzingatie maslahi ya wananchi na si maslahi binafsi ya kisiasa.

Leo ni siku ya mwisho kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupokea mapendekezo ya kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi.

Februari 26, mwaka huu Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele alisema tume hiyo inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Namba 2 ya Mwaka 2024.

Jaji Mwambegele alisema vigezo vitakavyotumika ni wastani wa idadi ya watu, kwa majimbo ya mjini ni kuanzia wastani wa watu 600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia wastani wa watu 400,000.

Alitaja vigezo vingine ni hali ya kiuchumi ya jimbo, ukubwa wa eneo la jimbo, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, uwezo wa ukumbi wa Bunge, idadi ya wabunge wa Viti Maalumu Wanawake, upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya eneo linalokusudiwa kugawanywa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Haji Semboja alisema hakuna tatizo katika jambo hilo ikiwa lengo la kugawa jimbo ni kurahisisha huduma kwa wananchi katika sehemu husika.

Profesa Semboja alisema anaunga mkono ugawaji wa majimbo unaofuata sheria na taratibu zilizopo kwa sababu katiba na sheria zinaangalia maslahi ya wananchi kwa kurahisisha utoaji wa huduma za kijamii katika jimbo husika.

Alihimiza wabunge wanaochaguliwa majimboni kufanya kazi kwa bidii kuwaondolea taabu wananchi katika maeneo ya kiutawala kama kata, vijiji na vitongoji.

Mwanasiasa mkongwe Paul Kimiti aliitahadharisha serikali na kuitaka kuwa macho na kazi ya ugawaji wa majimbo ili isiwe kazi ya kisiasa zaidi badala yake iwe ya kuwanufaisha wananchi kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Ugawaji wa majimbo unatakiwa uwe na ujumbe na maelekezo kwa wabunge kwenda kuwatumikia wananchi na usiwe mchakato wa kutafutia watu fulani nafasi katika siasa,” alisema Kimiti huku akihimiza mchakato wa kugawa majimbo uzingatie sheria za nchi na si kubebana katika siasa.

Naibu Katibu Mkuu Zanzibar wa Chama cha ACT Wazalendo, Salim Bimani alisema chama hicho kinaunga
mkono ugawaji wa majimbo kwa sababu lengo ni kuwasaidia wananchi katika kupata maendeleo.

Bimani alisema ugawaji wa majimbo utaongeza tija katika huduma zinazoelekezwa kwa wananchi ikiwamo kuongeza
idadi ya watetezi wa wananchi pamoja na kurahisisha huduma kwa wananchi.

Mkazi wa Msamvu mjini Morogoro, Selemani Chande alisema ugawaji wa majimbo ni hatua nzuri ya kupeleka huduma za kijamii karibu na wananchi.

Alitoa mfano wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki kuwa linastahili kugawanywa kutokana na ukubwa wake hali inayokwamisha huduma bora kwa wananchi wake.

“Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki limeanzia Ngerengere hadi Kisarawe mpaka kwenye Bwawa la Kidunda mkoani Pwani. Watoto wanapata shida kutokana na umbali wakati wa kwenda shule,” aliongeza Chande ambaye mwaka 2000 aligombea ubunge katika jimbo hilo kupitia chama cha NCCR – Mageuzi.

Alisema ikiwa jimbo hilo litagawanywa itakuwa afadhali kwa wananchi wake kwa sababu watapata ahueni katika sekta ya elimu na afya kwani kutajengwa hospitali na vituo vya afya katika jimbo jipya na kuwa msaada kwa wananchi.

Juzi Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam iliridhia ombi la kugawa Jimbo la Ukonga kuwa majimbo mawili
ya Ukonga na Kivule.

Kwa kuzingatia pendekezo hilo Jimbo la Ukonga litabaki na kata saba ambazo ni Ukonga, Pugu, Pugu Stesheni, Gongo la Mboto, Zingiziwa, Buyuni na Chanika.

Jimbo la Kivule litakuwa na kata sita za Msongola, Majohe, Kitunda, Kipunguni, Kivule na Mzinga.

Kwa kuzingatia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Jimbo la Kivule litakuwa na watu 431,736 na Jimbo la Ukonga litakuwa na watu 459,810.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button