Mawakili wa serikali wafundwa maslahi ya taifa
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amesema ofi si yake imeweka mkakati wa kuwajengea umahiri mawakili wa serikali katika kuishauri serikali vizuri kwa maslahi ya taifa, usalama wa taifa na uchumi endelevu
katika sekta mbalimbali.
Johari amesema hayo wakati akitoa salamu za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mawakili takribani 300 wa serikali wanaoshiriki mafunzo ya siku tano yaliyoandaliwa na ofisi yake jijini Arusha.
Alisema eneo la mafunzo wanalipa umuhimu mkubwa katika kuwajengea umahiri mawakili hao ili ushauri wanaoutoa uisaidie serikali kufanya uamuzi sahihi bila kuingia katika migogoro na mtu au watu au taasisi nyingine.
“Lengo kubwa la mafunzo haya ni kukuza ubora wa kisheria kwa maendeleo endelevu. Tunataka ubora katika huduma za sheria uwe mzuri ili kuleta maendeleo kwa taifa letu, ndiyo maana tunawajengea umahiri. Sekta ya sheria ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa katika sekta mbalimbali kama vile viwanda, biashara na nyinginezo,” alisema Johari.
Aliongeza: “Hakuna kitakachofanyika bila kuwa na sheria mahususi iliyotungwa kwenye eneo husika au mkataba fulani wa kibiashara, ili kuwe na mikataba na miradi mikubwa, sekta zinazokua kiuchumi, lazima kuwe na sheria mahususi kwenye sekta mahususi kama kilimo, usafirishaji, SGR, Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, biashara, nishati, madini na nyinginezo”.
Hata hivyo, alisema Johari alisema kuna ugonjwa umewakumba mawakili wa kuchelewa kufanya kazi zinazowapasa na kuziahirisha hali inayoweza kuchangia Tanzania kutofikia uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.
Alisema ubora katika huduma za sheria unamtaka mwanasheria kufanya kila jambo kwa wakati bila kuchelewa ikiwemo kufika eneo husika kwa wakati na kutoa huduma kwa wakati na kwa kuzingatia ubora.
“Imekuwa changamoto kwa nchi nyingi za Afrika na zinazoendelea watu kuwa goigoi katika utoaji huduma, hivyo kaulimbiu yetu ya weledi na ubora itakuwa ngumu kuifikia kama hatutafanya kazi kwa haraka na kwa wakati. Usipofanya kazi kwa wakati unajizalishia ugonjwa wa kuchelewachelewa na kuahirisha mambo bila sababu ya msingi, na matokeo yake wateja wanakosa huduma,” alisema Johari.
Alisisitiza: “Huduma zisipotolewa zinakuwa na athari katika biashara, ukuaji wa uchumi; hivyo, pamoja na mafunzo haya kuongeza umahiri wetu katika sheria, pia tunataka kunoa mfumo fikra wetu kwa kufanya kazi kwa haraka na ubora bila kuchelewa. Tunataka hilo tulivae kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kufanya kazi kwa haraka na kwa ubora”.
Naye Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole aliwapitisha mawakili hao katika maeneo mbalimbali ya kisheria ambayo wanapaswa kuyazingatia katika kutoa ushauri sahihi kwa serikali bila kuzua taharuki.
Mwanasheria mstaafu, Sirilius Mafupa aliwasisitiza mawakili hao kuzingatia weledi katika uandishi wa ushauri na uwasilishaji wa huo ushauri kwa wadau.
“Tumesisitiza wawe mahiri kisheria, wajue tatizo wanalolitolea ushauri, waliwasilishe kwa weledi kwa kutumia lugha rahisi inayoeleweka na wadau au mdau husika na wajitahidi kutotumia lugha ya kukera au yenye maudhi, kwa kufanya hivyo, ushauri utamfikia mdau kama ulivyo na utamsaidia kutatua changamoto aliyonayo,” alisema.
Mwandishi Mkuu wa Sheria Msaidizi-Urekebu na Mratibu wa Mafunzo, Rehema Katuga alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ana jukumu kubwa la kuishauri serikali katika masuala ya kisheria ikiwamo mikataba, ununuzi, uandishi wa sheria, sheria mpya zinazotungwa na mambo mbalimbali yanayohusu shughuli za serikali.
Katuga alisema kupitia mafunzo hayo wanataka kuongeza umahiri kwa mawakili kuondoa changamoto ambazo serikali inaweza kupitia ikiwamo kuvunjwa kwa mikataba na mikataba kutosimamiwa vizuri ili kuongeza umahiri na tija kwa serikali.



