Makamu wa Rais mgeni rasmi uzinduzi mbio za mwenge kitaifa

MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mbio za mwenge kitaifa utakaofanyika Aprili 02 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema hayo mjini Kibaha mara baada ya kufanya ukaguzi wa maandalizi ya uzinduzi huo  na kwamba maandalizi yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.

Amesema baada ya mbio hizo kuzinduliwa, mgeni huyo rasmi atawakabidhi viongozi sita wa mbio za mwenge walioandaliwa kutoka Tanzania bara na Zanzibar jukumu la kuukimbiza katika mikoa 31 yenye jumla ya halmashauri 195 kwa siku 195.

Kikwete amesema mwenge wa Uhuru utafanyakazi ya kuhamasisha amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa sambamba na kuhimiza wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yao.

Ujumbe wa mbio za mwenge 2025 ni,  “Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu” na kwamba umelenga kuwaelimisha na kuwakumbusha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

“Sambamba na ujumbe huu pia umelenga kuwaelimisha wananchi kupambana na maradhi yanayotishia ustawi wa watu wetu yakiwemo ukimwi, malaria na kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya rushwa,”alisema.

Kikwete ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Pwani na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi wakati wa uzinduzi huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button