Mashirika ya umma kwenda kimataifa

SERIKALI imezitaka taasisi na mashirika ya umma ambayo hayajajisajili kwenye masoko ya mitaji ya kimataifa kufanya hivyo ili kuwezesha wananchi kuyamiliki kwa sehemu kwa kununua hisa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo alisema hayo mjini Kibaha mkoani Pwani jana wakati akifungua mkutano wa pili wa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.

“Serikali ina hisa chache katika kampuni 56 na baadhi yake zinatoa gawio kwa serikali, sasa ni lazima kampuni zetu ambazo serikali ina umiliki ambazo bado hazijaingia kwenye masoko ya kimataifa ya mitaji zifanye hivyo,” alisema Profesa Kitila.

Aliongeza: “Ziingie masoko ya Afrika na kimataifa na baada ya miaka mitano hadi kumi tuzione kwenye ushindani ziwe miongoni mwa kampuni kubwa zenye ushindani katika Ukanda wa Afrika na duniani kwa ujumla”.

Alisema hadi sasa kampuni 10 za Kitanzania zilizosajiliwa kwenye masoko ya mitaji ya kimataifa zinafanya kazi nje ya nchi, ingawa alibainisha idadi hiyo ni ndogo na inapaswa ziongezeke.

“Uchumi wa dunia unaendeshwa na kampuni na sisi tunatamani kuona kampuni zetu zikiingia huku,” alibainisha Profesa Kitila.

Alisema serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi.

Aidha, alisema taasisi za umma ambazo hazijajisajili kwenye masoko hayo ya mitaji zifanye hivyo ili kutoa fursa kwa wananchi kununua hisa na umiliki.

Aidha, aliyataka mashirika na kampuni hizo kuja na mikakati ya kuongeza faida, ushirikiano na sekta binafsi, pamoja na kuoainisha mikakati yao ya kibiashara, vipaumbele vya serikali na Mpango wa Taifa wa Maendeleo.

Akizungumzia kampuni ambazo serikali ina hisa chache na hazitoi gawio serikalini, Profesa Kitila alisema ni lazima zijiulize kwa nini hazitoi gawio licha ya kuwa ni kampuni za kibiashara na waone kuna haja ya kubadilika na kufanya kazi ili kupata faida na kutoa gawio serikalini.

“Ninatoa changamoto kwenu kutimiza majukumu yenu kama wakurugenzi wa kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache,” alisema Profesa Kitila.

Aliongeza: “Tunapaswa kuja na mikakati thabiti ambayo itaboresha utendaji wa kampuni zilizo chini ya uangalizi wetu”.

Profesa Kitila alitoa wito kwa watendaji wa kampuni hizo kuendelea kujifunza mifumo ya teknolojia mpya ya kidijiti ili kupunguza mawasiliano ya ana kwa ana.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambazo kati ya hizo, 56 ni zile ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.

Katika kampuni hizo chache 56 serikali imewekeza jumla Sh trilioni 2.8 na Sh trilioni 83.4 zikiwekezwa na serikali kwenye taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100.

“Tunataka tuone matunda ya uwekezaji huu na ndio maana nawataka mfanye kila liwezekanalo kuongeza ufanisi wa taasisi zenu,” alisema Profesa Kitila, huku pia akizishukuru taasisi ambazo tayari zinachangia vizuri katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Tausi Kida alisema kuna changamoto mpya kwa wafanyabiashara na serikali imeziona na kuagiza watendaji wazitafutie ufumbuzi.

Alisema katika hilo siku chache zijazo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atazindua Mpango Mpya wa Ufanyaji Biashara na Uwekezaji unaoendana na Mazingira ya Sasa (MKUMBI).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button