Kada CCM asifu utendaji wa Rais Samia

ALIYEKUWA Kamanda wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kada wa chama hicho, Justine Nyari amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi wa mfano wa kuigwa na kuwataka watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao kumuombea afya njema ili aendelee kufanya kazi vizuri.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumzia miaka minne ya utendaji wa Rais Samia.

“Tumeona mageuzi na maboresho makubwa katika sekta za kilimo, afya, madini, utalii, umeme, maji, elimu, viwanda, mazingira na hata diplomasia ya kimataifa, amefanya mambo ambayo baadhi ya watu duniani wanajiuliza Rais Mwanamke amewezaje kufanya mambo yote haya tena kwa miaka michache tu madarakani,”alisema Nyari.

Alisema katika utawala wake wa miaka minne, Rais Samia pia ameboresha sekta ya elimu kwa kuongeza madarasa, nyumba za walimu, kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kubadili mfumo wa elimu ili watoto waweze kufundishwa masomo ya kuwawezesha kujitegemea na elimu bure kwa kila mtanzania.

Pia alisema maboresho hayo katika sekta ya elimu ndio yaliyomvutia yeye pia kuwekeza kwa kujenga Shule ya Msingi ya Glisten Pre & Primary School iliyoko Mirerani wilayani Simanjiro ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika sekta hiyo.

” Mama amekuwa akihamasisha uwekezaji, hasa kwa watanzania, binafsi kama mfanyabiashara na kada wa CCM niliamua kuunga mkono jitihada za Rais wetu kwa kujenga shule hapa Mirerani, watoto wetu wanafaulu na wengine kupangiwa shule za vipaji maalumu kama Ilboru, Tabora Girls, Msalato na nyinginezo,” alisema.

Kuhusu sekta ya madini, alisema Rais Samia anastahili pongezi kwa uwekezaji uliofanywa na serikali yake katika sekta hiyo ikiwemo kujenga jengo la kuuzia madini ambapo wafanyabiashara na wanunuzi watalitumia kufanyabiashara na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri mbali kutafuta masoko.

“Mirerani tumejengewa jengo kubwa lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano, hapa kutakuwa na ofisi za madini, hivyo wanunuzi kutoka pande mbalimbali duniani na ndani ya nchi watakuwa wakija hapa kununua madini, ule mnada wa Jaipur India sasa utakuwa hapa, na huu unaenda kuwa mji wa madini hasa,” alisema.

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, alisema Rais Samia hana mpinzani anayeweza kumsema vibaya kutokana na maendeleo makubwa aliyoyafanya nchini kwa ajili ya watanzania.

Kuhusu kauli ya upinzani kutaka kugomea uchaguzi, Nyari alisema anaamini watanzania wote wataenda kupiga kura na hakutakuwa na mgomo wowote.

“Kuhusu ubunge, kwa utaratibu wa CCM ambaye mimi ni miongoni mwa makada wake, kuna utaratibu tunatakiwa kuufuata, na ukizingatia majimbo takribani yote bado yana wabunge tena wanatokana na CCM, hivyo haturuhusiwi kutangaza chochote hadi muda utakapofika,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button