Bunge la Israel lapitisha sheria tata

ISRAEL : BUNGE la Israel limepitisha leo sheria inayowapa viongozi waliochaguliwa mamlaka zaidi katika kuwateua majaji, hatua iliyosababisha upinzani mkali kutoka kwa vyama vya kisiasa vya mrengo wa kati na kushoto.
Sheria hiyo iliidhinishwa kwa kura 67 dhidi ya moja, huku upande wa upinzani ukikusudia kuzuia kikao hicho cha asubuhi kwa kususia.
Bunge la Israel lina wabunge 120, na kura hii inaonyesha azma ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuendelea na mpango wake wa mageuzi ya mahakama, ambao ulizua maandamano makubwa nchini Israel mwaka 2023 kabla ya kuibuka kwa vita vya Gaza.
Baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, kiongozi wa chama cha Yesh Atid, Yair Lapid, alitangaza kupitia mtandao wa kijamii wa X kuwa amekata rufaa katika mahakama ya juu dhidi ya sheria hiyo kwa niaba ya vyama vya upinzani, akisema kuwa hatua hiyo inapingwa vikali na wengi.
Waziri wa Haki, Yariv Levin, ambaye alileta muswada wa sheria hiyo, alieleza kuwa lengo la hatua hii ni kudumisha usawa kati ya nguzo kuu za serikali, hasa kati ya bunge na mahakama, ili kuhakikisha kuwa hakuna upande mmoja unapata nguvu kubwa kuliko mwingine.
Sheria hii imezua mjadala mkubwa kuhusu huru wa mahakama na ushawishi wa kisiasa katika uteuzi wa majaji, jambo ambalo linatarajiwa kuendelea kuwa kipengele kikubwa cha mjadala nchini Israel.
SOMA: Jeshi la Israel lashambulia Gaza



