Samia: Tuwajibike

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kukuza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma ili kuleta utawala bora.

Rais Samia amesema hayo Ikulu, Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU).

Alisema ukaguzi uliofanywa na CAG unatoa taswira ya matokeo ya hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuziimarisha taasisi za umma.

“Taasisi hizi mbili CAG na Takukuru zitaendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na uzalendo wa hali ya juu kwa manufaa ya taifa letu. Sisi upande wa serikali tupo tayari kuendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa ndani ya taarifa hizo mbili,” alisema Rais Samia.

Alisema jitihada zinafanywa kuziimarisha taasisi za umma ili ziweze kutumia vizuri rasilimali za umma.

Rais Samia alisema serikali imepata faraja kwa sababu matokeo ya ukaguzi huo yameonesha kwa ujumla kuna kuongezeka kwa ufanisi kwenye matumizi ya rasilimali za serikali.

Alisema pamoja na mapungufu yaliyotajwa na CAG, mapungufu mengi ni ya kipindi cha nyuma lakini kwa kuangalia mwendelezo kumekuwa na ufanisi kwenye matumizi ya rasilimali za serikali.

“Hiyo ni faraja yetu kama serikali kwamba tumeweza kukuza uwazi, uwajibikaji na hatimaye kuleta utawala bora na tunaendelea kuleta utawala bora ndani ya serikali,” alifafanua Rais Samia.

Alisema taarifa ya Takukuru imeashiria kuongezeka kwa ufanisi kwa njia mbili ambazo ni ufanisi ndani ya Takukuru yenyewe akibainisha katika kipindi cha miaka sita iliyopita taarifa ya Takukuru inakuwa na maswali mengi.

Rais Samia alisema taarifa ya sasa ya Takukuru imeonesha wanafanya kazi kwa kupunguza mapungufu yao binafsi na sasa wanafanyakazi kuendana na taratibu husika na ndio maana wameweza kuyaona mengi na kuyafanyia kazi.

Alitaja jambo la pili kuwa taarifa imeonesha kukua kwa ufanisi ndani ya taasisi za umma huku ikionesha kuwa Tanzania imepanda kutoka nafasi iliyokuwepo kwenye mapambano dhidi ya rushwa na kupanda ambayo ni ishara nzuri kuwa kuna kitu kizuri kinafanyika ndani ya taasisi za umma.

Alisema serikali itaendelea kusikiliza na kufuatilia vizuri mjadala wa bunge kwenye taarifa ya CAG huku akiahidi
kuifanyia kazi vizuri taarifa ya Takukuru yale yote yaliyoelezwa ndani ya taarifa hiyo ili kujenga utawala bora ndani ya nchi.

Alisema ripoti ya Takukuru imeonesha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja
na mifumo ndani ya taasisi za umma kitu kilichosababisha kupungua kwa kasoro zilizokuwa zikijitokeza awali.

“Takukuru wametuambia kuna kiwango kikubwa cha kukuza ufahamu na kujenga ujasiri kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla kufahamu rushwa ni nini na kujenga ujasiri wa kuisema,” aliongeza.

Alisema jambo lingine ambalo ni kubwa kuliko ni kujenga uelewa dhidi ya rushwa kwa vijana wa shule za msingi mpaka vyuo jambo alilolitaja kama tija kwa sababu itawasaidia vijana kukua katika utamaduni wa kuichukia rushwa hata watakapoingia ofisini watakuwa na utamaduni huo.

Aliipongeza Ofisi ya CAG kwa kufanya kazi kubwa yenye manufaa kwa taifa, ikiwemo kuchunguza ufanisi wa miradi mbalimbali, ikiwemo mifumo ya Tehama katika taasisi za umma.

Rais Samia amemuomba Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuipokea na kuiwasilisha bungeni kwenye mkutano unaofuata na kuifanyia kazi kwa wakati na akaahidi serikali itazipitia kwa makini taarifa hizo na kuzifanyia kazi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button