Takukuru yabaini Takukuru yabaini kasoro 5 kodi ya zuio
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imebaini kasoro tano katika mfumo wa ukusanyaji na uwasilishaji wa kodi ya zuio katika halmashauri.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila amesema hayo Ikulu Dar es Salaam kabla ya kumkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan taarifa ya utendaji kazi ya mwaka 2023/2024.
Chalamila alitaja kasoro hizo ni usimamizi hafifu, halmashauri kutowajibika, kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu kinachotakiwa kupokelewa kutoka halmashauri na halmashauri kutokuwa na kumbukumbu sahihi za hundi za kodi ya zuio zilizoidhinishwa.
Alitaja kasoro nyingine ni kukosekana mfumo wa pamoja unaoratibu utekelezaji wa miradi ngazi ya halmashauri jambo ambalo linaipa ugumu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuratibu kodi ya zuio na hivyo kutoa mwanya wa ufujaji wa mapato husika.
Chalamila alisema Takukuru ilifanya kazi 660 za utafiti na uchambuzi wa mifumo ya utoaji huduma kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna bora ya kuziba mianya iliyobainika.
Alisema taasisi hiyo imefanya uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji na uwasilishaji wa kodi ya zuio katika halmashauri 101 nchini kwa lengo la kutathmini ufanisi wa mfumo huo.
Kwa mujibu wa Chalamila malengo mahususi yalikuwa ni kutathmini ukusanyaji wa kodi ya zuio: uwasilishaji wa kodi ya zuio TRA na mifumo ya ndani ya udhibiti katika ukusanyaji na uwasilishaji wa kodi hiyo.
Alisema ulibainika halmashauri 52 kati ya 101 zilizofikiwa zinakata kodi ya zuio kutoka kwa wazabuni mbalimbali.
“Kati ya halmashauri zinazokata kodi hiyo, halmashauri 41 zinawasilisha kodi kikamilifu na halmashauri 11 zinawasilisha kodi pungufu” alisema Chalamila.
Alisema baada ya kazi ya Takukuru halmashauri 35 kati ya 49 ambazo zilikuwa hazijawasilisha kodi hiyo zimeiwasilisha kodi husika TRA.
“Kiasi ambacho kilikuwa hakijawasilishwa kwa halmashauri zilizofikiwa na uchambuzi ni Shilingi milioni 186.3 kwa mwaka wa 2021/22 na Shilingi bilioni 1.38 kwa mwaka 2022/23, hivyo baada ya ‘intervention’ (kuchukua hatua) ya Takukuru, kiasi cha Shilingi bilioni 2.15 kilikusanywa na kuwasilishwa TRA,” alisema Chalamila.
Alisema ili kuboresha ukusanyaji wa kodi ya zuio kuna pendekezo la kuunganisha mifumo ili malipo yoyote ya miradi yanayofanywa katika ngazi ya vituo na halmashauri yaratibiwe na kodi husika kuwasilishwa Chalamila alisema pia, kuna pendekezo la kuimarisha ufuatiliaji wa ukataji na uwasilishaji wa kodi ya zuio na kuimarisha mkakati wa utoaji elimu juu ya ulipaji, ukusanyaji na uwasilishaji wa kodi ya zuio kwa wadau wote.
Pia, alisema Takukuru imefanya ufuatiliaji wa rasilimali za umma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo 1,773 ya thamani ya Sh trilioni 11.48.
Chalamila alitaja miradi hiyo ni ujenzi wa hospitali za rufaa katika mikoa ya Songwe; Katavi; Kigoma; Singida;
Geita na Tabora; ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato, Dodoma; urejeshwaji wa mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri na matumizi ya fedha za mfuko wa afya.



