Mwenge wa Uhuru kuwashwa leo

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango leo anatarajiwa kuwasha Mwenge wa Uhuru Kibaha mkoani Pwani.

Dk Mpango anatarajiwa kuwasha Mwenge katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha na unatarajiwa kukimbizwa katika mikoa 31 na halmashauri 195 nchini.

Jumapili iliyopita, Majaliwa alisema anaamini halaiki imepata mafunzo mazuri na inawezekana ikawa ndiyo halaiki nzuri kuliko zote kutokana na maandalizi mazuri.

“Nimeona vijana wameiva na wanaonesha jinsi walivyokuwa wakakamavu na wana ari kubwa ya kufanya halaiki hiyo siku itakapofika na wanatia matumaini makubwa,” alisema Majaliwa.

Majaliwa aliagiza wenyeji waalike mikoa jirani ikiwemo ya Dar es Salaam, Morogoro na Tanga, makundi mbalimbali, watu maarufu na shule za msingi na sekondari za Pwani kwa kuwa hilo ni jambo la kitaifa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete alisema vijana wakimbiza mwenge kitaifa walikuwa tayari na vifaa vyao.

Ridhiwani alisema wageni 16,000 watakaa kwenye viti na mafunzo kwa vijana na watu mbalimbali yametolewa kutambua falsafa za Mwenge wa Uhuru.

Wakati wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka jana mkoani Mwanza, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alimpongeza, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia na kuendeleza falsafa ya Mwenge wa Uhuru katika misingi ya muasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Dk Mwinyi alisema mwenge ulikimbizwa katika mikoa yote 31 kuhamasisha na kudumisha umoja, amani, uzalendo, kuhamasisha maendeleo na kudumisha Muungano wa Tanzania.

Mbio za Mwenge kwa mwaka jana zilikagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo 1,595 yenye thamani ya Sh trilioni 11.02 kwa siku 195 nchini kote.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka jana, Godfrey Mnzava alisema kati ya miradi hiyo, 16 yenye thamani ya Sh bilioni 8.6 ilikataliwa kutokana na kukutwa na kasoro.

Mnzava alisema waliikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nyaraka za miradi hiyo kwa uchunguzi na hatua stahiki.

Alipendekeza kwa Rais Samia Suluhu Hassan aagize mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2025 zizindue miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.

“Halmashauri chache nchini zinazotumia mapato ya ndani kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi, halmashauri nyingi hazina maelezo yanayoridhisha juu ya matumizi ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani yanayokusanywa hasa katika eneo hili la utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi,” alisema Mnzava.

Aliongeza, “ikitokea Rais ukaelekeza mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2025, zishughulikie miradi ya maendeleo inayotekelezwa na mapato ya ndani ya halmashauri zetu hapa nchini, watu watakimbia halmashauri zao.”

Alipendekeza mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zifuatilie mpango wa usambazaji wa nishati vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwa utekelezaji wake ni kero katika maeneo mengi nchini.

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka jana zilizinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Aprili 02 mkoani Kilimanjaro.

Imeandikwa na John Gagarini (Kibaha) na Eva Sindika (Dar es Salaam).

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button