UNFPA, Finland watakiwa kuwafikia wengi

DAR-ES-SALAAM : WITO umetolewa kwa Serikali ya Finland na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi (UNFPA) kuendelea kufadhili awamu nyingine ya mradi wa Chaguo langu, Haki yangu kuzifikia wilaya nyingi nchini na kuhakikisha jamii ya Tanzania inakuwa salama.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam leo na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto  Zanzibar Abeida Rashid Abdallah katika mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa mradi huo uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu kwa mafanikio.

Amesema  licha ya mafanikio bado kuna wanawake na wasichana wengi, hasa walioko nje ya maeneo ya utekelezaji wa mradi, wanaoendelea kukumbwa na ukatili wa kijinsia, mila kandamizi na ukosefu wa huduma za kijamii na afya ya uzazi.

“Mradi huu umekuwa msaada mkubwa kwa utekelezaji wa sera na mikakati ya kitaifa, ukiwemo mpango kazi wa kupambana na udhalilishaji wa wanawake na watoto (NPA-VAWC II 2025-2030), mpango wa maendeleo ya Zanzibar (ZADEP 2020-2025) pamoja na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050, bado tunawahitaji” amesema.

Amepongeza serikali ya Finland kwa kushirikiana na (UNFPA) kwa kufadhili na kutekeleza mradi huo unaolenga kulinda haki na chaguzi za wanawake na wasichana, hususan wenye ulemavu nchini.

Mwakilishi mkazi wa UNFPA Mark  Schreiner, ameishukuru serikali ya Finland, akisema mradi huo umekuwa  muhimu kwa kufikia mustakabali ambapo wanawake na wasichana wote wanaishi kwa amani, uhuru, na usawa.

Amesema mradi huo unaunga mkono juhudi za kitaifa za kupambana na ukatili wa kijinsia (GBV), ndoa za utotoni na ukeketaji, kupitia mbinu ya sekta mbalimbali.

Naibu Mkuu wa Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Finland nchini Sanna Taivalmaaa, amesema dhamira ya Finland ni kuona usawa wa kijinsia kama kipengele muhimu cha sera zao za kigeni.

Amesema Finland imejitolea kukuza afya na kukomesha ukatili wa kijinsia, kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake na wasichana wenye ulemavu.

Amepongeza mradi huo kwa kuwawezesha wasichana na wanawake  kupinga kanuni hatari za kijamii na kuimarisha huduma kwa kushirikiana na mamlaka za mitaa na mashirika yanayosaidia watu wenye ulemavu.

Mratibu wa mradi huo, Rashida Sharrif, amesema mradi huo umegharimu jumla ya  dola za kimarekani  milioni 6.9. Hapo awali, walipewa dola milioni 6.2, na baadaye dola milioni 1.7 ziliongezwa.

SOMA: Rais Samia kuzindua ripoti ya tafiti afya ya uzazi na mtoto

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button