Tanzania yaorodheshwa Daraja la Kwanza miongoni mwa nchi 46 duniani ulinzi wa kimtandao

ARUSHA: USALAMA na uaminifu katika masuala ya kidijitali yametajwa kuwa msingi katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali dhidi ya changamoto za usalama wa kimtandao na ulinzi wa taarifa za binafsi za watumiaji wa mitandao nchini na kimataifa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini (ICTC), Dk Nkundwe Mwasaga wakati akifungua Jukwaa la Nne la Usalama wa Kimtandao la Tanzania 2025 jijini Arusha jana linalokutanisha kwa siku mbili washiriki takribani 200 wa ndani na nje ya nchi.
Dk Mwasaga alisema Tanzania imejikita katika nguzo kuu tano ili kufikia mageuzi makubwa ya kidijitali ikiwemo kukuza ujuzi wa kidijitali, usalama na uaminifu katika masuala ya kidijitali, huduma za mawasiliano ya kidijitali, kujenga uchumi wa kidijitali, kufanya tafiti za kidijitali, ubunifu na ujasiriamali katika masuala ya kidijitali.
Alisema kutokana na nguzo hizo tano, Tanzania imeanza kupata mabadiliko chanya katika masuala ya kidijitali na usalama wa kimtandao ikiwemo kutumia na kufaidika na teknolojia na majukwaa ya kidijitali kuufanya uchumi wa Tanzania kuwa wa ushindani zaidi.
“Nguzo ya usalama na uaminifu wa kidijitali ni muhimu sana. kwa sababu hii ndiyo nguzo inayozungumzia kuhusu usalama wa kimtandao na ulinzi wa taarifa binafsi, huo ndiyo msingi wa uaminifu tunapojenga uchumi wa kidijitali unaohusisha watu wengi,”alisema Dk Mwasaga.
Aliongeza” Hivyo jukwaa kama hili linalofanyika mara moja kwa mwaka ni muhimu kwetu kwa kuwa linatupa fursa ya kuwasikiliza wataalamu wetu wa TEHAMA wa ndani na nje ya nchi ili kujadili mambo ambayo ni muhimu kwa nchi yetu.”
Dk Mwasaga alisema kwa mujibu wa ripoti ya kimataifa ya masuala ya kimtandao (GCI) 2024, Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa kuorodheshwa kwenye Daraja la Kwanza miongoni mwa nchi 46 duniani zinazofanya vizuri katika masuala ya ulinzi wa kimtandao ambayo ni nafasi ya juu zaidi duniani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, alisema kila ukanda duniani una nchi ambazo ni mfano wa kuigwa au zinazoendelea, na kila ukanda una nchi ambazo ziko katika hatua za mwanzo za kujenga usalama wa mtandao.
Naye Kamishna wa Ulinzi wa Taarifa za Mtandaoni kutoka Ujerumani, Dk Tino Nauman pamoja na mambo mengine, alisema kuwa anatambua Tanzania ina sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi kama ilivyo Ujerumani na nchi nyingine ambalo ni jambo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali.
Alisema taarifa yoyote inayomhusu mtu binafsi, kisheria hiyo ni taarifa binafsi kama vile umri wa mtu au namba ya utambuzi, mawasiliano ya mtu na mtu, barua pepe na mengineyo.
Baadhi ya washiriki akiwemo Sarah Mwaisumo, Mhadhiri Msaidizi Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) alisema katika kuhakikisha wanafunzi wao wanakuwa wabobezi kwenye masuala ya ulinzi wa mtandao, serikali imewekeza maabara ya kisasa ya TEHAMA chuoni hapo.
Alisema maabara hiyo inawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo masuala ya kidijitali ikiwemo ulinzi wa taarifa na usalama wa kimtandao ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.



