Tril 3.5/- bado hazijalipwa mashirika ya umma

DODOMA — Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amefichua kuwa mashirika ya umma 106 nchini yana madai ya muda mrefu yanayofikia Sh trilioni 3.58, yakihusisha huduma mbalimbali zilizotolewa kwa wateja.

Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi ya Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imebaini ongezeko kubwa kutoka trilioni 2.92 mwaka uliopita, hali inayodhoofisha uwezo wa mashirika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

CAG ametoa mifano kadhaa ya mashirika yenye changamoto kubwa, yakiwemo Bohari ya Dawa (bilioni 267.79), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (bilioni 180), na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ambayo deni lake limefikia bilioni 931.14. Pia Shirika la Nyumba la Taifa linakabiliwa na wadaiwa waliotoroka na madeni ya zaidi ya bilioni 19 bila kulipa.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa baadhi ya taasisi kama Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kutoa huduma kwa taasisi zisizolipa madeni yao, kinyume na sera, jambo linaloathiri utoaji wa huduma bora za afya. Vilevile, kuna madeni yasiyo hai yenye thamani ya Sh bilioni 35.21 katika mashirika mbalimbali, huku sababu kubwa zikitajwa kuwa ni usimamizi dhaifu wa ankara, kumbukumbu duni za wateja, na ufuatiliaji hafifu.

CAG amependekeza mashirika hayo kuboresha mifumo ya udhibiti wa ndani, kufanya maridhiano ya hesabu, na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wadaiwa sugu.

Pia amesisitiza kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya ni muhimu ili kuimarisha mtiririko wa fedha na uendelevu wa mashirika ya umma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button