Ustawi wa jamii watakiwa kutatua changamoto kidijitali

DAR ES SAALAM: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk John Jingu amewataka wanafunzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii kutumia mbinu za kidigitali na teknolojia inayokua kwa kasi kila siku.

Dk Jingu pia amewataka waalimu katika chuo hicho kuendana na mazingira ya sasa ya dunia kwa kujitahidi kufundisha kidigitali na teknolojia mpya.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa ziara chuoni hapo kukagua miradi na maendeleo, Dk Jingu amesema matumizi ya akili mnemba yanahusika katika ustawi wa jamii kwa kiasi kikubwa hivyo wanafunzi wajitahidi na sio kila kitu kujifunza darasani.

“Ninavutiwa na kazi mnazofanya mlizonieleza kama uanagenzi, ubunifu, dawati la jinsi mnafanya vizuri ,nyie ni mainjinia wa kutengeneza jamii na mara nyingi mnakutana na mwanajamii akiwa na shida na mtoa kutoka chini na kunyanyua juu baada ya kupata matumaini.

Amesema maafisa ustawi ni daraja la changamoto na suluhu au majawabu katika jamii hivyo ubunifu wao ni mzuri zaidi kwa ustawi wa jamii.

“Kituo cha ubunifu kinazaa matunda ni jambo kubwa kuna changamoto nyingi katika jamii ila kila changamoto ni mwaliko wa kufanya suluhu nzuri zaidi nimeona mmefanya changamoto kuwa ni fursa na muendelee kufanya changamoto kuwa fursa”,ameeleza.

Amebainisha kuwa lengo la ubunifu sio tu kutatua changamoto bali kuleta vitu vipya ambavyo vitatumika katika jamii ambapo sasa kuna changamoto kubwa ya afya ya akili duniani.

“Hali si nzuri mtu usiku usingizi ukiwa umeisha anakimbilia simu kuna watu wanauraibu wa mitandao kuna mtu anaendesha gari halafu anachati ,kuna urabu wa dawa za kulevya,ukatili,migogoro ya familia,migogoro ya kazi maisha kubadilika kwa mtu yanayoleta msongo wa mawazo.

Aidha amesema suala la ukatili liendelee kutafutiwa mbinu mpya ya utatuzi kwani kuna wanaume na wanawake wanafanyiwa ukatili, na watoto na wazee hivyo pia waimarishe ubunifu, unasihi na uanagenzi.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo,Dk Joyce Nyoni amesema taasisi inafanya miradi mbalimbali ya kitaalamu ambapo wamesomesha wahadhiri watatu na wanafunzi 10 kupitia miradi.

“Wanafunzi 30 walifanya mafunzo kwa vitendo ndani ya jamii kuangalia changamoto zao mikoa ya Tanga ,Mtwara na Iringa tulifanya kazi na wazee ambao jamii inawaongelea vibaya.

Aidha ameomba wizara iwape bajeti  kufanya maboresho na pia waongezee nguvu wanapoongea na wafadhili na wadau ili kufikia makubaliano.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button