Ripoti utendaji BBT kutolewa kila mwaka

SERIKALI inatarajia kuanza kutoa ripoti ya kila mwaka ya Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kuonesha kilichofanyika kwa wanawake na vijana kwa mwaka mzima katika maeneo mbalimbali kupitia mradi huo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ataizindua rasmi ripoti hiyo Aprili 27 jijini Dodoma ikihusisha mambo mbalimbali kwenye sekta ya kilimo kwa upande wa serikali na sekta binafsi.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika mkutano wa wadau wanaotekeleza miradi ya kuwezesha vijana na wanawake katika sekta ya kilimo-mazao uliofanyika jana jijini Dodoma.

Bashe alisema wanafanya hivyo ili kuonesha maendeleo yaliyofanyika na wizara ya kilimo kwenye sekta ya kilimo kwa mwaka mzima kupitia vijana wa BBT na sekta nyingine zinazohusu kilimo, lakini pia na wanawake ambao wamewezeshwa kwenye kilimo.

Alisema uzinduzi wa ripoti hiyo utaenda sambamba na maandalizi ya uzinduzi wa benki ya ushirika Aprili 28 kwa ajili ya kuanza kuwanufaisha wakulima na wafanyabiashara nchini.

“Tumepanga kutoa ripoti kila mwaka ya mradi wa BBT, tunaizindua rasmi Aprili 27, mkakati huo utaendelea kila mwaka ili kuijulisha jamii nini serikali inafanya kitu gani katika mradi wa BBT,” alisema Bashe.

Alisema ripoti ambayo itazinduliwa na kuanza kutolewa kila mwaka, itasaidia jamii kujua nini kinaendelea katika mradi wa BBT ambao unahusisha vijana na wanawake kwa ajili ta kujiinua kiuchumi kupitia kilimo wanachofanya.

Aidha, alisema pia mradi huo una manufaa makubwa sana kwa wananchi hususani vijana na wanawake, wengi wao sasa hivi wananufaika na kilimo cha umwagiliaji na wengine cha matunda pamoja na mazao ya chakula.

Bashe pia, aliwapongeza wadau wa sekta ya kilimo wanaotekeleza miradi ya kuwezesha vijana na wanawake katika sekta ya kilimo kutokana na kuunga mkono juhudi za serikali kwenye sekta ya kilimo hapa nchini.

Alisema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika ukuzaji wa kilimo hususani kwenye kilimo cha umwagiliaji ambapo wanaendelea kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za umwagiliaji ili kuhakikisha wakulima wanapiga hatua.

Naye Msajili wa vyama vya Ushirika, Revocatus Nyagilo alisema makubaliano waliyosaini kwa ajili ya kuendelea kusaidia vijana kwenye sekta ya kilimo yatasaidia kuzidi kupanua wigo wa kilimo kwa upande wa rika hilo.

Nyagilo amesema ushirika huo wa pamoja ni moja ya mkakati wa kuwainua vijana na wanawake kujikita kwenye kilimo ili kuhakikisha wanajiinua kiuchumi wao na familia zao lakini pia watachangia pato la taifa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button