Samia: Tunabeba ndoto za Nyerere

DODOMA; RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Sita na zilizopita zimefanikiwa kutekeleza kwa vitendo maono na fikra za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere zilizokuwa na malengo ya kumuinua mwananchi.
Pia, alitoa wito kwa wananchi kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana kuleta maendeleo katika taifa.
Rais Samia alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Mwalimu Julius Nyerere na safari yake katika Picha iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma wakati wa maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema serikali zote ziliendeleza maono na mipango ya dira ya taifa ya maendeleo kwa kufanya kazi na ni muhimu kazi hizo ziendelezwa na kuenziwa.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) katika awamu tofauti tumeendelea kumuenzi mwalimu kwa kutekeleza yale aliyokuwanayo kama dira ya mipango ya maendeleo,” alisema.
Aliongeza: “Serikali imeendea kutekeleza fikra zake katika kutekeleza miradi na kuleta maendeleo katika taifa letu na kulitunza jina la JMT (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) huko ulimwenguni… tunafanya hivi kwa kuimarisha Muungano wenyewe na kutatua changamoto zinazoweza kukwamisha shughuli za muungano”.
Alisema, Nyerere alikuwa na maono ya kuona elimu inayotolewa inaendana na maisha ya Watanzania na kuwawezesha vijana wanaohitimu kujitegemea.
Alisema 2024, serikali ya awamu ya sita ilianza utekelezaji wa sera ya elimu iliyoboreshwa, iliyoweka msisitizo kwa wanafunzi kujengewa ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa.
Katika sekta ya kilimo, Rais Samia alieleza kuwa serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika kilimo iliyochangia kuongeza akiba ya mazao na nchi kujitosheleza kwa chakula huku kukishuhudiwa na ongezeko la mauzo ya mazao nje ya nchi.
Pia, kwa upande wa vijana, serikali imetekeleza miradi inayotoa fursa za kilimo, uvuvi na ufugaji wa kisasa.
Alisema serikali imeendelea kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo iliyokuwa na mchango katika jamii, akitolea mfano mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHEPP) na Bwawa la Kidunda ambalo ujenzi wake ulifikia asilimia 50 na Bwawa la Mkomazi litakaloongeza tija katika kilimo cha umwagiliaji.
Alisema serikali imeendelea kudumisha ushirikiano wa kikanda na ushirikiano wa kimataifa na kutekeleza mpango wa serikali kuhamia makao makuu ya nchi Dodoma.
Aidha, kwa upande mwingine alisema serikali ilitekeleza jitihada za kukuza lugha ya Kiswahili na kuifanya kujulikana kikanda na kimataifa.
Alisisitiza kuwa Mwalimu Nyerere ameacha alama isiyofutika na kupitia historia yake katika ujenzi wa taifa, inawapa ujasiri na uthubutu viongozi katika kujenga nchi.
Rais Samia alisema serikali inaendelea kuimarisha muungano kwa kutatua changamoto zinazokwamisha muungano ili kuwaenzi waasisi wa muungano na kutunza jina la Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Akimzungumzia Nyerere, alisema kupitia kitabu hicho kinawakumbusha Watanzania kupambania ujenzi wa taifa jumuishi lisilo na ubaguzi.
Alisema, Mwalimu Nyerere alionesha uzalendo kwa vitendo, alisimamia misingi ya maelewamo na aliamini kuwa nguvu ya Tanzania ipo katika umoja na mshikamano wa watu wake.
Aliweka wazi mchango wa wanawake wakati wa Nyerere uliosaidia kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Alihimiza kuwa kitabu hicho kilichozinduliwa ni sehemu ya historia na kuenzi muungano.
Jana, Tanzania iliadhimisha miaka 61 ya muungano katika kila mkoa ikiambatana na kaulimbiu isemayo: ‘Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa: Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.’



