BBT yazidi kunoga

SERIKALI imezindua mradi wa mashamba makubwa utakaotekelezwa kwa miaka mitano kwa gharama ya dola za Marekani takribani milioni 241.27 (Sh bilioni 646).
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imefadhili kwa mkopo wa Dola za Marekani milioni 129.91 ambazo ni asilimia 53.79 ya gharama za mradi huo na Serikali ya Tanzania itachangia asilimia 46.21 za gharama za mradi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua mradi huo Dodoma jana ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).
Majaliwa alisema tangu kuanzishwa kwa programu ya BBT serikali imekuwa ikitafuta wadau wa maendeleo kwa ajili ya kushirikiana katika utekelezaji wake hasa katika eneo la upatikanaji wa rasilimali fedha.
Alisema AfDB imekubali kufadhili utekelezaji wa mradi huo kwa kutoa mkopo wa masharti nafuu wenye riba ya asilimia 0.2 kupitia BBT awamu ya kwanza utakaotekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030.
Majaliwa alisema mradi huo utafanya kazi za maendeleo ndani ya vyama vya ushirika, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa dirisha la kuwezesha kifedha vijana na wanawake.
“Dirisha hili litasimamiwa kupitia Benki ya Ushirika kwa kushirikiana na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF),” alisema.
Majaliwa alisema mradi huo unatarajiwa kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuongeza ajira, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, na kuinua uchumi wa vijana nchini Tanzania.
Alisema kupitia mradi huo wakulima vijana 11,000 watawezeshwa sambamba na biashara za kilimo takribani 6,000 zinazomilikiwa na vijana.
“Pia vijana wengine 2,500 ambao tayari wanajishughulisha na kilimo biashara lakini hawana sifa za kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha, watawezeshwa kupata mitaji kwa ajili ya kukuza shughuli zao,” alisema Majaliwa.
Pia, amezindua Programu ya Kuimarisha Kanda za Kukuza Kilimo (AGCOT) ambayo imelenga kuongeza uzalishaji na ufanisi katika Sekta ya Kilimo kwa kutumia mbinu shirikishi zinazozingatia hali halisi ya kijiografia na ikolojia ya maeneo mbalimbali nchini.
“Lengo kuu la mpango huu ni kuhakikisha kuwa kila eneo la kilimo nchini linapangwa na kuendelezwa kulingana na hali ya hewa, aina ya udongo, na sifa nyingine muhimu za kijiografia,” alisema Majaliwa.



