Tanzania yataka Umoja Afrika kukabili tabianchi

SERIKALI ya Tanzania imesema ni muhimu kundi la majadiliano la viongozi wa Afrika (AGN) liwe na sauti moja ili kupata mikakati ya kupata fedha za kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika mkutano uliokutanisha kundi la timu ya viongozi wa AGN Unguja

Dk Mpango alisema mabadiliko ya tabianchi ni janga Afrika na duniani kwa ujumla hivyo inahitajika mikakati ya pamoja mbele ya washiriki wa maendeleo na taasisi kza kifedha ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la kimataifa (IMF).

Kwa mfano alisema kwa upande wa Tanzania chini ya rais Dk Samia Suluhu Hassan anaongoza kwa kubeba ajenda ya kampeni ya nishati safi ya kupikia ya gesi ambayo lengo lake kubwa kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo ukataji wa miti.

Aidha, alisema kampeni hiyo imeanza kupata mafanikio makubwa yanayotokana na ushawishi ambapo ifikapo mwaka 2030 matarajio kwa asilimia 80 wananchi wawe tayari wanatumia nishati hiyo.

“Suala la mabadiliko ya tabia ya nchi na njia ya kukabiliana nazo tayari limeanza kutekelezwa kikamilifu kwa upande wa jamhuri ya muungano ambapo matarajio ifikapo mwaka 2030 kuona kwamba kwa asilimia 80 wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia,” alisema.

Akizungumza Mwenyekiti wa kamati ya wajumbe wa kundi la viongozi wa Afrika (AGN) ya kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi Richard Muyungi alisema wamekuta hapo kwa ajili ya kuja na mikakati ya pamoja na mambo muhimu ambayo wataiwasilisha katika mikutano muhimu ya kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu huko Brazil pamoja na Berlin Ujerumani.

“Mkutano huu malengo yake ni kuweka mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na wenzetu hapa wapo wafadhili wakubwa wanaotubeba ili tuwe na sauti moja mbele ya mikutano ya kimataifa kwa ajili ya kuomba ufadhili wa misaada mbalimbali,” alisema Muyungi ambaye ni mshauri wa Rais katika masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi.

Akizungumza Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa kwanza wa Rais Harusi Said Suleiman amesema Zanzibar ikiwa kisiwa tayari kipo katika tishio kubwa la athari za mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo juhudi za kukabiliana na athari hizo zimeanza kuchukuliwa.

Kwa mfano alisema Serikali imetenga bajeti katika kila wizara kushughulikia mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo kampeni ya kuirudisha Zanzibar kijani ambayo inahusisha zoezi la kupanda miti kwa wingi.

“Mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake ni kubwa ambapo Zanzibar na sisi hatuko salama huku tukichukua juhudi mbalimbali kukabuiliana na changamoto hizo ikiwemo kuirudisha Zanzibar ya kijani kuotesha miti kwa wingi,” alisema.

Naibu Mkurugenzi wa Mazingira katika Idara ya Mabadiliko ya Tabianchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Dk Kanizio Manyika alisema wameanza kuchukua juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa Zanzibar pamoja na Ukanda wa Pwani wa Tanzania kuanzia Tanga hadi Mtwara.

Alizitaja juhudi hizo ikiwemo ujenzi wa ukuta katika mkoa wa Tanga kufuatia kasi ya maji ya bahari kuja juu na kutishia makazi ya wananchi pamoja na maeneo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano tumeanza kuzifanyia kazi changamoto zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zaidi katika ukanda wa Bahari ya Tanzania kuanzia Tanga hadi Mtwara pamoja na Zanzibar kwa ujumla,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button