Tucta yasifu madai yao kutimizwa

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mkoani Singida.
Maadhimisho hayo yanafanyika yakiwa na kaulimbiu: “Uchaguzi Mkuu 2025, utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi, sote tushiriki”.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeipongeza serikali kwa kutekeleza madai ya wafanyakazi.
Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alisema usikivu wa serikali umeongeza kiwango cha malipo ya mkupuo ya pensheni kwa wastaafu kutoka asilimia 33 ya sasa mpaka asilimia 40.
Nyamhokya alilieleza HabariLEO kuwa nyongeza hiyo ni kwa wafanyakazi waliokuwa wanapokea asilimia 50 kabla ya mifuko kuunganishwa na asilimia 35 kwa watumishi ambao walikua wakipokea asilimia 25 kabla mifuko hiyo kuunganishwa.
Pia, alisema Tucta inafurahia uamuzi wa serikali kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa wazazi waliopata watoto njiti hadi kufika wiki 40 huku baba akiongezewa muda wa likizo kutoka siku tatu hadi saba.
“Jambo lingine ambalo tunaishukuru serikali ni kwa kudhamiria kuendelea kutekeleza mikataba ya kimataifa ya wafanyakazi ambayo kimsingi inalenga kuwatetea na kulinda wafanyakazi, tunashukuru kwa hilo,” alisema Nyamhokya.
Alisema pia serikali Tucta inashukuru serikali imetekeleza madai yao ya muda mrefu ya kuongeza kikokotoo akisisitiza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia nyongeza hiyo itapanda hadi kufika asilimia 50.
“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio hiki cha muda mrefu cha watumishi, ameonesha mapenzi yake kwetu. Ni matumaini yetu kwamba baada ya mwanzo huu mzuri basi hali itakapokaa sawa asilimia hizi zitaongezeka kufikia 50,” aliongeza Nyamhokya.
Alitaja mambo mengine yaliyotekelezwa kwa asilimia kubwa ni ajira mpya serikalini kwa kuwa maelfu wafanyakazi wameguswa zikiwemo zilizotokana na mikakati ya serikali katika kilimo, mikopo na nyinginezo na kusaidia wananchi kupata kipato.
Nyamhokya aliiomba serikali kuwasaidia wafanyakazi ambao hawajapanda vyeo na madaraja wapande ili kufaidi utumishi wao pamoja na kuendelea kushusha kodi za mishahara ili kipato cha wafanyakazi kiongezeke.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU), Joseph Mwitwa alisema madai mengi ya wafanyakazi yamefanyiwa kazi yakiwemo kupanda madaraja kwa watumishi.
“Tunaishukuru serikali kwa usikivu wake kwani madai mengi yametekelezwa kama nyongeza ya mishahara ya kila mwaka sasa inatolewa, kuthibitisha watumishi waliokuwa wakikaimu nafasi kwa muda mrefu na kulipa malimbikizo ya wafanyakazi,” alisema Mwitwa.
Alisema kitendo cha kuwathibitisha watumishi katika nafasi walizokaimu kinawajenga watumishi kisaikolojia na kuongeza morali ya kazi kwani mtumishi anayekaimu muda mrefu bila kuthibitishwa anakosa kujiamini na hawi mbunifu.
Aliiomba serikali itekeleze madai ya wafanyakazi ambayo bado hayajatekelezwa kama vile kuendelea kupunguza kodi ya mishahara ya watumishi na kupandisha kima cha chini cha kukata kodi kutoka chini ya 370,000 hadi milioni moja.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Joseph Misalaba alisema Rais Samia anastahili pongezi kwa namna alivyowajali na kuwathamini walimu nchini katika eneo la maslahi.
Misalaba alisema baada ya kuona matatizo ya walimu yamekuwa mengi, serikali iliunda chombo cha kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za walimu kijulikanacho kama ‘Samia Teachers’ Mobile Clinic’ kilichozunguka nchi nzima katika mikoa 26 na kuwezesha utatuzi wa changamoto mbalimbali za walimu.
“Chombo hicho kinajumuisha Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais Tamisemi, Ofisi ya Rais Utumishi, Wizara ya Elimu na Tume ya Utumishi ya Walimu na kuwezesha malimbikizo mbalimbali ya walimu pamoja na mishahara kulipwa,” alisema.