Mauaji ya mtoto yamuibua wakili: “Tukimrejea mungu, ukatili utakwisha”

IRINGA: Tukio la kusikitisha na kutisha lililotokea hivi karibuni mjini Iringa, ambapo mwanaume anadaiwa kumuua na kumkatakata vipande mtoto wake wa kumzaa, limetikisa jamii na kuibua mjadala mpana kuhusu ukatili dhidi ya watoto na nafasi ya jamii katika kulikomesha janga hilo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari na kuthibitishwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, mtuhumiwa wa tukio hilo ni Joseph Yustino Muhulila ,28, mkazi wa Mtaa wa Lukosi, Kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa anadaiwa kumuua mtoto wake, Timotheo Joseph Muhulila .6, kwa kumkata viungo na kutupa mabaki ya mwili wake kwenye shimo la choo, tukio lililotokea usiku wa Aprili 12, 2025.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, alisema awali mtuhumiwa aliripoti kuwa mtoto wake alipotea, lakini maelezo yake yalileta mashaka makubwa, hali iliyosababisha uchunguzi wa kina kufanyika.
Mei 6, mwaka huu, Polisi walifanikiwa kumbana kwa mahojiano ya kina ambapo alikiri kutenda mauaji hayo.
Kamanda Bukumbi alieleza kuwa baada ya tukio hilo la kutisha, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi wa eneo hilo walifanikiwa kuopoa mabaki ya mwili wa mtoto huyo kutoka katika shimo la choo, japo yakiwa yameharibika vibaya.
Katika uchunguzi wa awali, imebainika kuwa mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa mama yake aliyekuwa naye baada ya wawili hao kuachana, kwa nia ya “kumtembelea.”
Wakati jamii ikiendelea kushangazwa na kuguswa na tukio hilo la kinyama, wakili wa kujitegemea na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Moses Ambindwile, amesema kuwa matukio kama haya hayawezi kuepukika ikiwa jamii itaendelea kumwacha Mungu.
“Tukimrejea Mungu hatuwezi kukafanya ukatili wa namna hii. Huu ni ushetani uliopitiliza. Tukimrejea Mungu tutakuwa na upendo,” alisema Ambindwile.
Aliongeza kuwa mizizi ya baadhi ya matukio haya ya ukatili mara nyingi husababishwa na imani za kishirikina na jamii isiyo na hofu ya Mungu.
Hata hivyo amesisitiza kuwa mfumo wa kisheria nchini unaendelea kufanya kazi kwa ufanisi katika kulinda haki za watoto na kupambana na ukatili wa kijinsia.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha haki za watoto zinalindwa. Taasisi kama TLS tunatoa huduma kwa wahanga wa ukatili na pia tunatoa elimu ya kisheria kwa jamii.”
Ambindwile amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema kila wanapobaini viashiria vya ukatili, ili kuokoa maisha ya watoto wasio na hatia kama Timotheo.
Alisema tukio hili linajenga hoja kubwa juu ya nafasi ya jamii, familia, taasisi za kidini, na viongozi wa kijamii kushirikiana kuzuia chimbuko la ukatili wa namna hii.
“Ni wakati wa kila mmoja kutafakari na kuchukua hatua – kabla maisha mengine hayajapotea kwa mikono ya wazazi wao wenyewe,” alisema.



