Madiwani watakiwa kuhamasisha wananchi uboreshaji daftari kura

MKUU wa Wilaya yaTandahimba mkoani Mtwara, Kanali Michael Mntenjele amewataka madiwani wa halmashauri hiyo kuwahamasisha wananchi wajitokeze kwenye uboreshaji wa daftari la kudumu la wapira kura awamu ya pili ili kuhakiki usahihi wa taarifa zao kwenye vituo vya uandikishaji.
Ameyasema hayo wakati wa kikao cha kawaidia cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kuhusu kupitia taarifa mbalimbali za halmashauri robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo.
Aidha wananchi hao wanaotakiwa kuhakiki taarifa hizo katika zoezi hilo linalotarajiwa kuanza rasmi mkoani humo Mei 16 hadi Mei 22, 2025 ni wale waliyokosa kujiandikisha awamu ya kwanza wa zoezi hilo wakiwemo vijana.
Sambamba na hilo mkuu huyo wa wilaya ameendalea kuwasisitiza madiwani hao kuendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwenye kata zao iliyowekezwa fedha nyingi na serikali.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo pia ni diwani wa kata ya kitama, Baisa Baisa ametilia makazo suala hilo la madiwani hao kuhusu miradi kuwa, wahakikishe fedha hizo zilizotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zinatumika kama ilivyokusudiwa.
‘’Kuna fedha zimewekwa kwenye akaunti za vijiji kwenye kata zenu, hakikisheni fedha hizo zinatekeleza miradi iliyokusudiwa ili iweze kukamilika kwa wakati, kama mna changamoto katika utekelezaji wa hii miradi msikae kimya shirikisheni idara husika’’amesisitiza Baisa.
Baadhi ya madiwani hao akiwemo wa kata ya Nanhyanga Abbas Namaneha, ameipongeza na kuiomba serikali kuongeza kasi ya usambazaji wa pembejeo za korosho ili mkulima wa zao hilo azipate kwa wakati.
Usambazaji wa pembejeo hizo unaendelea kwenye maeneo mbalimbali yanayolima korosho nchini kwa msimu wa kilimo mwaka 2025/2026.



