Kwaheri shujaa Msuya

SAFARI ya maisha ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa David Msuya (94) imehitimishwa jana alasiri katika kijiji alichozaliwa cha Chomvu, Usangi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, alikozikwa kwa mazishi ya kitaifa.

Msuya aliyezaliwa Januari 4, 1931 kijijini hapo, alikuwa Waziri Mkuu kwa vipindi viwili tofauti katika awamu mbili tofauti.

Kwa mara ya kwanza, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu Novemba 7, 1980 hadi Februari 24, 1983 chini ya Rais Mwalimu Julius Nyerere na aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais kuanzia Desemba 5, 1994 hadi Novemba 27, 1995 chini ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Alifariki dunia Mei 7, mwaka huu kwenye Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya moyo.

Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza waombolezaji kumzika kiongozi huyu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na kisha Waziri wa Viwanda, Fedha, Uchumi na Mipango na Viwanda na Biashara, na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda na mageuzi ya kiuchumi katika awamu ya kwanza na ya pili.

Wakati wa ibada ya maziko katika Kanisa la Kristo Mchungaji Mwema Usangi, wilayani hapa, Rais Samia alisema ujumbe mkubwa wa Msuya ulikuwa kuhimiza viongozi wawe na uthubutu katika kuwatumikia wananchi.

Rais Samia alisema, Msuya ameacha hadithi nzuri aliyoiandika katika maisha yake ambayo ina mambo mengi ambayo viongozi wa sasa wana ya kujifunza.

Alitaja mambo muhimu manane kutoka kwa Msuya ambayo aliwakumbisha viongozi wa sasa na wajao kuwa ni muhimu kuyashika.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kusimamia katika mambo ambayo viongozi wanayaamini na kuyasimamia kwa nguvu zote na kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uadilifu kitu ambacho, Mzee Msuya alitekeleza kwa moyo wake wote.

Sambamba na hayo, alisema jambo la tatu Msuya aliamini kuwa ujuzi na utaalamu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Rais Samia alisema Msuya hakuwa mwoga wa mabadiliko hata kidogo na kwamba aliamini kuwa mabadiliko ni msingi wa maendeleo kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema katika utumishi wake, Msuya anatuma ujumbe wa umuhimu wa uvumilivu katika utumishi wa umma kama unavyoelezewa vizuri katika Falsafa ya 4R ya Rais Samia.

“Jambo la sita ambalo linapatikana katika utumishi wa mzee wetu ni kujenga umoja na mshikamano kwa taifa kama alivyofanya kwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga,” alisema Rais Samia akimuelezea kiongozi huyo aliyepewa jina la Baba wa Mwanga.

Rais Samia aliagiza kukamilishwa kwa Kituo cha Afya cha Chomvu kama ishara ya kutekeleza mambo aliyotamani yakamilike kwa masilahi ya maisha ya wana Mwanga.

“Mzee Msuya alianzisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Chomvu na hakijakamilika, tutahakikisha kinakamilika kwa mchango wa kila mtu pamoja na mimi,” alieleza.

Alisema serikali itaendelea kumuenzi na kuchota busara zake katika kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na uzalendo.

Rais Samia alieleza namna, Msuya alivyofurahishwa kutokana na kukamilika kwa baadhi ya miradi inayotekelezwa na serikali wilayani Mwanga ukiwamo Mradi wa Maji wa Mwanga – Same – Korogwe pamoja na Barabara ya CD Msuya.

Alisema mwaka 2010 alionana na Msuya ana kwa ana wakati wa kampeni wilayani Mwanga na Same alipokwenda kupata ushauri kuhusu upinzani uliokuwepo wakati huo.

Rais Samia alieleza kuwa anashukuru kwa kumzika, Msuya huku akiwa amekamilisha Mradi wa Maji wa Same – Mwanga – Korogwe, na kwamba Mradi wa Barabara ya CM Msuya unaendelea kutekelezwa.

“Mzee Msuya atakumbukwa kwa mengi ambayo yamesemwa na wengi sana waliofanya naye kazi. Atakumbukwa kwa kuyatoa maisha yake yote kuwatumikia Watanzania,” aliongeza Rais Samia.

Alisema wakati wote wa maisha yake, Msuya hakutumia maisha yake kwa mambo binafsi bali kutumikia taifa. Alieleza kuwa ameweka rekodi ya kipekee kwa kuwa waziri aliyeitumikia nafasi hiyo kwa muda mrefu kuliko wote.

Rais Samia alimtaja pia, kama shujaa aliyeongoza mabadiliko ya mfumo wa uchumi ili kuruhusu uchumi huria ili kuokoa uchumi wa taifa.

“Miaka ya 1980 na 1990 kulikuwa na harakati za kuishusha thamani Shilingi ya Tanzania… nakumbuka tukiwa wanafunzi ‘tuliimba Msuya usiruhusu Shilingi ishuke thamani,” alikumbusha Rais Samia.

Alisema hata Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kupitia kitabu chake cha ‘Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yangu,’ alimtambua Mzee Msuya kama kielelezo cha mageuzi ya uchumi.

Aliongeza kuwa, Msuya atakumbukwa pia kwa juhudi zake za kutafuta fedha za kuunga mkono harakati za ukombozi wa Afrika akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

Mbali ya uongozi wa kiserikali, Agosti mwaka 1995 Msuya alikuwa miongoni mwa wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopigiwa kura ya uteuzi wa kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 1995. Alishindwa na Benjamin Mkapa aliyeibuka kidedea. Mwingine alikuwa Jakaya Kikwete.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button