Mikakati kuboresha mazingira sekta ya utalii iungwe mkono

MKUTANO wa Tatu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na sekta ya umma na binafsi katika utalii unaendelea jijini Arusha ukiwa na lengo la kujadili maendeleo ya sekta ya utalii nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utalii.
Mkutano huo pia ni mwendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).
SOMA: Tanzania mwenyeji jukwaa la kimataifa utalii wa vyakula
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana, wizara yake ina dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta ya utalii ili ichangie kikamilifu katika uchumi na maendeleo ya taifa.
Na katika hili anabainisha kuwa dhamira pia inaenda sambamba na utekelezaji wa malengo ya kimkakati ya uendelezaji na utangazaji utalii, ambako wizara imeendelea kutekeleza mikakati ya kukuza utalii ikiwamo kuimarisha utoaji wa huduma.
Mikakati hii ya wizara kwa hakika ni muhimu kutokana na ukweli kuwa sekta ya utalii imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, kutokana na Tanzania kujaliwa vivutio vingi vya utalii.
Tumeshuhudia juhudi kubwa zikifanywa na serikali na Rais Samia Suluhu Hassan binafsi katika kuhakikisha sekta ya utalii inapiga hatua kubwa.
Rais Samia ameshiriki katika filamu mbili maarufu nchini ‘Tanzania: The Royal Tour’ na ‘Amazing Tanzania’, ambazo pamoja na mikakati mingine, zimeongeza idadi ya watalii kufikia 5,360,247 wakiwamo watalii wa ndani 3,218,352 na wa nje 2,141,895.
Mbali ya ongezeko hilo la watalii, pia mapato yatokanayo na shughuli za utalii yamefikia Dola za Marekani bilioni 3.3, huku Tanzania ikitambuliwa katika sekta ya utalii duniani kuwa miongoni mwa zinazofanya vizuri ikiwa kuwa na watalii wengi.
Kwa msingi huu, mkutano huu wa Arusha ni muhimu katika kuendeleza kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta ya utalii, ili kuifanya mchango wake katika Pato la Taifa uzidi kuongezeka na kuchangia kiasi kikubwa katika maendeleo.
Tunaamini ushirikishwaji wa sekta binafsi ni muhimu katika eneo hilo kwani inachukua sehemu kubwa katika maendeleo ya sekta hasa eneo la uwekezaji na miundombinu ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuboresha mazingira ya sekta.
Ni mategemeo yetu kwamba wadau hawa wataweka mikakati inayotekelezeka kutumia Sera ya Taifa ya Utalii katika kuhakikisha wanafikia lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta hii, ambayo ikitekelezwa, Tanzania itaendelea kuvuna mengi katika sekta ya utalii na kuimarisha ustawi wa wananchi.