Kongole uongozi wa Rais Samia kufungua milango haki jumuishi

KATIKA kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya Katiba na Sheria imeendelea kushuhudia mabadiliko makubwa yanayolenga kuimarisha misingi ya haki, utawala bora na heshima kwa sheria.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro inathibitisha kuwa serikali imeweka juhudi madhubuti kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwamba sheria haziishii kwenye makabrasha ya kisheria bali zinakuwa nyenzo ya maisha ya kila Mtanzania.
Tunaungana na Watanzania wote kupongeza hatua hizi ambazo zimeleta mageuzi chanya yanayoendana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025.
Elimu ya katiba, uraia na utawala bora iliyowafikia wananchi zaidi ya milioni sita ni ushahidi wa dhahiri kwamba serikali imeamua kujenga msingi imara wa ushiriki wa wananchi katika masuala ya kisheria na kidemokrasia.
Hili ni jambo la kujivunia, hasa kwa taifa linaloendelea kujenga utamaduni wa kushirikisha wananchi katika maamuzi ya msingi yanayohusu maisha yao.
Kwa upande mwingine, tafsiri ya sheria 300 kwa lugha ya Kiswahili ni hatua muhimu inayolenga kuhakikisha sheria zinaeleweka kwa wananchi wa kawaida.
Hii inaendana na azma ya Rais Samia ya kuhakikisha haki haisomeki kwa watu wachache bali inafika kwa wote.
Aidha, marekebisho ya sheria 57 na zaidi ya sheria ndogo 4,000 ni kielelezo kingine cha kazi kubwa iliyofanyika katika muda mfupi mchakato ambao unahitaji kuungwa mkono na wadau wote.
Tunapongeza pia uamuzi wa serikali kuanzisha Sera ya Haki Jinai na kuimarisha miundombinu ya utoaji haki, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa ofisi za mashitaka katika wilaya 108 kati ya 139 nchini, na kuajiriwa kwa watumishi 600.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania imepunguza kwa kiwango kikubwa mrundikano wa mashauri mahakamani hadi kufikia asilimia nne pekee ya mashauri yanayodumu kwa zaidi ya mwaka. Hili ni jambo la kihistoria na la kujivunia Afrika.
Kupitia utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, serikali imeonesha kuguswa na mahitaji ya wananchi wa kawaida, hususani wanawake na makundi maalumu. Kampeni hii inaonesha wazi kwamba uongozi wa Rais Samia umejengwa juu ya misingi ya huruma, haki na usawa.
Sisi tunaamini mafanikio haya ni matokeo ya dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga Tanzania yenye misingi imara ya haki, amani na mshikamano.
Tunatoa wito kwa wadau wote wa sheria, mashirika ya kiraia na wananchi kushirikiana na serikali kuhakikisha
mafanikio haya yanakuwa endelevu.