Samia ataka umeme wa nyuklia

RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza viongozi watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia viapo wakati wanaapishwa.
Alisema hayo Ikulu Dar es Salaam jana baada ya kuapisha viongozi akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Fred Msemwa na Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Dk Blandina Kilama.
Profesa Tumaini Nagu ameapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya afya na Jaji mstaafu John Mgetta ameapishwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili.
“Hata mimi nina nakala ya kiapo changu nakaa kipindi kisha naichukuwa naitazama najiwekea alama wapi niko sawa wapi nalegea ndiyo maana ya kiapo hichi mnapewa nakala,” alisema Rais Samia.
Amemuagiza, Twange asimamie mradi wa uzalishaji wa umeme wa nyuklia kwa kutumia madini ya uranium yanayopatikana Tunduru mkoani Ruvuma.
Rais Samia alisema kwa muda mrefu nchi imekuwa na madini hayo lakini hayajatumika kama chanzo cha uzalishaji wa umeme.
“Kwa makadirio ya sasa hivi ni takribani tani 58,500 za uranium zimelala pale nadhani wakianza kuchimba na kufanya ugunduzi kwenye eneo lile wanaweza kupata mengi zaidi,” alisema.
Aliongeza: “Huu mradi uanze umeme wa nyuklia kama wao wanautumia tunaweza kuutumia tukawa na umeme wa kutosha nchi na kuuza nchi jirani kamna tunavyotaka kuuza sasa kwa Zambia”.
Pia, Rais Samia alisema Tanesco ni usalama wa nchi na serikali imewekeza kwenye uzalishaji wa nishati hiyo kwenye vyanzo tofauti ukiwemo Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Maji katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) na akasema mradi huo ndiyo roho ya nchi.
“Tuna umeme wa kutosha, Chalinze pale tuna umeme wa kutosha, tatizo tulilonalo ni ‘transmission’ (usafirishaji) kwenda kupeleka Kaskazini na huku wanaita Nyanda za Juu Kusini, miradi hiyo ipo lakini kulikuwa na kusuasua kwa kuanza kwa miradi hiyo,” alisema.
Aliongeza: “Kaangalie na ukakikishe usambazaji unafanyika kupeleka umeme kutoka kwenye gridi sehemu hizo, na kuna vyanzo vidogovidogo vinavyotoa umeme maeneo kadhaa ya Tanzania na yenyewe ukayatupie jicho vizuri. Tanesco kama nilivyosema ni usalama wa nchi’’.
Rais Samia alisema hadi kufikia sasa vijiji vyote nchini 12,318 vimeunganishwa na huduma ya umeme na vitongoji 33,657 sawa na asilimia 52 vimeunganishwa na huduma ya umeme.
Alisema kazi ya kuunganisha vitongoji vingine 20,000 inaendelea na akasema miradi hiyo itasaidia kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Aidha, Rais Samia amemtaka Twange asimamie miradi kwa manufaa ya taifa na si watu binafsi na aondoe makandokando yanayofanywa na baadhi ya watumishi wa shirika hilo.
Tume ya Mipango
Rais Samia amemuagiza Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Fred Msemwa na Naibu wake, Dk Kilama waratibu miradi ya kitaifa kwa kuhakikisha inatekelezwa katika sehemu husika kwa ufanisi na kuhakikisha miradi ya kisekta nchini inafungamana na malengo ya kitaifa.
Alisema Watanzania wana imani kubwa na Tume ya Mipango na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo unawategemea wao.
Rais Samia ameiagiza tume hiyo iratibu miradi yote, ikiwemo mikubwa ya kitaifa ya uwekezaji.
“Ndiyo maana mmeitwa Tume ya Mipango, hakikisheni kila mradi unaokuja wa kitaifa umekaa pahali pake na unatekelezwa vilivyo kama tulivyokubaliana katika mikataba yetu.
“Dira (2050) iko hatua ya mwisho utekelezaji utawategemea nyinyi naomba mkasimame vizuri ni kipindi kizito na kigumu ambacho mmeingia lakini ni imani yangu kwamba mnaweza mkafanya vizuri,” alisema.
Maagizo kwa Profesa Nagu
Rais Samia amemuagiza Profesa Nagu asimamie kuondoa urasimu katika manunuzi kwa kusimamia sheria.
“Jitahidi kutafuta ufumbuzi wa shida za wananchi kule chini na mkaondoe urasimu usio na tija kwa michakato ya manunuzi na jitahidini mkazingatie sheria,” alisema.
Alisema katika kipindi cha kati ya 2020 na 2025 kumekuwa na ongezeko la vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya na mikoa.
Rais Samia alisema pia serikali imekarabati hospitali kongwe nchini sambamba na kupeleka watumishi wa afya na vifaa tiba katika maeneo hayo.
“Lengo letu ni kuhakikisha afya ya msingi inaboreshwa na tunasogeza huduma karibu zaidi na wananchi, una kazi kubwa naomba uende ukasimamie,” alisema.
Tume ya Maadili
Rais Samia amemuagiza, Jaji Mgeta asimamia maadili ya viongozi wa utumishi wa umma na watumishi wa umma ili watekelekeze majukumu kwa weledi.
“Sisi viongozi ni wanadamu kuna miiko tumewekewa, ukitufanyia tathmini leo unaweza kutukuta ni asilimia 30 tu ndiyo tunaifuata hiyo miiko ya uongozi sasa mna kazi ya kutulea huko na kuangalia ujazaji tu fomu na kuwaleteeni… lakini matendo yetu mengine binafsi huku ni mambo mengine,” alisema.
Rais Samia alisema utumishi wa umma ni miongoni mwa injini zinazoiongoza nchi na akasema kuna baadhi wa watumishi wamekuwa wakikiuka miiko ya utumishi wa umma na kukosa uzalendo hadi kufikia hatua ya kutoa siri za maeneo wanayofanyia kazi.
“Leo hii mtumishi wa umma anakosa uzalendo anathubutu kuchukua siri katika mafaili akapiga picha katika simu yake na akaisambaza akijua kwamba anamkomoa Rais, akijua sijui anamkomoa nani sijui lakini kumbe ni yeye amekosa maadili, uzalendo kwa taifa lake hakuna,” alisema.
Rais Samia amehimiza wananchi walinde amani na utulivu wa nchi kwa kuwa makini na watu kutoka nchi za nje.
“Kazi ya kulinda amani sio ya kwangu peke yangu wala si vyombo vya ulinzi na usalama peke yao ni sote kwa sababu wakikosa huku watapita katika mawizara, mashirika yetu watataka wapite huko huko kutuvuruga, naomba mkalinde taifa lenu hii ndiyo rasilimali tuliyoachiwa hatuna nyingine nendeni mkailinde,” alisema.