Wakongwe wa soka waliokuwa mafukara wa kutupwa

UMASIKINI. Ukiutaja watu wanapeleka mawazo ya picha za nyumba ndogo zenye mapaa ya nyasi au majani na watu waliovaa nguo chafu zilizopasuka wakiwa hawana viatu.

Pengo kati ya matajiri na masikini linazidi kukua duniani, huku masikini wakipoteza matumaini ya kuuendea utajiri, licha ya kupewa moyo na wasanii wachache kwamba wao ni matajiri watarajiwa.

Ukweli ni kwamba wengi wao hubanwa kwenye mzunguko wa matatizo, wasiruhusiwe kutoka humo wala kupatiwa fursa za kuonesha uwezo wao.

Soka, hata hivyo, imewatoa wengi humo ambao vinginevyo leo wangekuwa mafukara wa kutupwa kama si wangekuwa wameshaipa kisogo dunia hii.

Hapa ni mifano ya wanasoka watano maarufu sana wa zamani, ambao walitopea kwenye ufukara na familia zao kabla ya kunyanyuka, kupiga boli, kupata utajiri na hadi sasa baada ya kustaafu wanaishi raha mustarehe.

Ronaldo de Lima

Ronaldo anayesemwa sana siku hizi ni yule nyota wa zamani wa Manchester Unite, Real Madrid, ambaye sasa yupo Falme za Kiarabu. Cristiano, ‘anayenuka’ fedha, lakini ninayemzungumzia hapa ni Mbrazili aliyezaliwa katika viunga vya mafukara vya Rio de Janeiro mwaka 1976.

Umasikini uliifunika familia yao hivyo kwamba hata alipopata fursa ya kuondoka kwenye mzunguko wa madhila hayo kwa kwenda kufanya majaribio na timu ya Flamengo baada ya kipaji chake kugundulika, alishindwa kwa kukosa nauli japo ya kupanda mwana punda.

Hata hivyo, hatimaye alifanikiwa baadaye mwaka 1993 kwa kujiunga na klabu nyingine -Cruzeiro. Alijua ilikuwa bahati ya mtende, akaitumia vyema kwa kujibidisha kwenye mazoezi na kutia nidhamu hadi akaja kuchezea klabu bora kama Barcelona, Inter Milan, Real Madrid na AC Milan.

Ronaldo aliachana na soka 2011 akiwa na klabu ya Corinthians, akiacha rekodi ya mabao 280 katika jumla ya mechi 384 alizocheza kwenye klabu mbalimbali. Kadhalika alichezea Timu ya Taifa ya Brazil mara 98 na kufunga mabao 62, akawa mchezaji bora wa dunia mara mbili, mchezaji wa mwaka wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) mara tatu na kuchaguliwa na mtandao wa ‘ Goal.com’ kuwa mwanasoka wa muongo.

Rivaldo
Mkongwe mwingine wa Brazil katika soka ni Rivaldo, ambaye kwa bahati mbaya sana familia yake ilikuwa katika ukata usiomithilika hivyo kwamba mwenyewe alikuwa na utapiamlo na unyafuzi, matatizo ya kiafya yaliyomsababishia kuwa na umbo la ajabu na pia kupoteza meno yake mengi. Alianza soka ya kulipwa akiwa na umri wa miaka 16 tu, na ni hapo alipoanza kuuaga umasikini.

Kutokana na jitihada zake, Rivaldo alitokea kuchezea klabu kubwa duniani, ikiwa ni pamoja na Barcelona alikocheza mechi 157 na kufunga mabao 86. Alichezea timu ya taifa mara 74 na kufunga mabao 34.

Rivaldo hakustaafu rasmi kutoka kwenye ulimwengu wa soka, bali aliacha tu kucheza alipofikisha umri wa miaka 40, baada ya kuwa ametunukiwa tuzo kwa kuwa mwanasoka bora wa dunia, mchezaji wa mwaka wa Fifa na pia mwanasoka bora Ulaya wa mwaka.

Diego Maradona

Huyu ni mmoja wa wachezaji bora zaidi katika ulimwengu wa soka, lakini ukisikia alivyokua, unaweza kurejesha hisia nyuma na kumwonea huruma, hata kama alikuja kuchezea fedha na umaarufu wake kwa kula dawa za kuongeza nguvu au za kulevya.

Maradona alikulia kwenye mji mdogo na wa hovyo wa Villa Fiorito uliokaliwa na mafukara wengi, na mwenyewe alikuwa akitumia chumba kimoja kidogo na ndugu zake saba. Hakuweza kupata elimu ya shule na kitu pekee alichojua akilini mwake ni soka.

Huyu ni mwanasoka pekee aliyepata kuweka rekodi ya dunia kwa ada za mikataba mara mbili, kwanza akiwa na Barcelona alikovunja rekodi kwa pauni milioni tano na pili alipokwenda Napoli kwa ada ya pauni milioni 6.9.

Alicheza mechi 492 na kufunga mabao 258 akiwa na klabu mbalimbali, akianza kucheza akiwa na umri wa miaka 21. Alicheza mechi 91 kwa taifa lake na kufunga mabao 34. Amecheza kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Fifa, ikiwa ni pamoja na zile fainali za 1986, akiwa nahodha wa Argentina waliowafunga Ujerumani kwenye fainali.

Maradona ni mmoja wa wachezaji watata zaidi dunia kupata kuona, akipata umaarufu zaidi kwa lile ‘Bao la Mungu’ alilofunga dhidi ya England, linalochukuliwa kuleta wakati mtata zaidi katika historia ya soka ya kisasa.

Pamoja na hayo, katika mechi hiyo hiyo alifunga bao la karne dhidi ya England na amepata pia kutawazwa na Fifa kuwa mchezaji mwenza wa karne wa Fifa. Maradona kwa sasa ni marehemu.

Roberto Carlos

Beki huyu wa zamani wa pembeni naye alikulia katika umasikini uliokithiri, yeye na wazazi wake wakiwa hawajui starehe kule Garca, Sao Paolo. Kwa mujibu wa mwandishi wa habari na wa vitabu, John Carlin, Carlos alikuja kupata mapaja mapana kwa sababu alikuwa akitumiwa kufanya kazi mfano wa maksai.

Alikuwa na baba yake shambani wakihenyeka kuhemea mlo kwa kuvuta au kusukuma au kuvuta majembe ambayo yalitakiwa yakokotwe na ng’ombe, hivyo kwa lugha nyingine alikuwa ‘maksai mwanadamu’, kwa sababu mashine hizo zilikuwa nzito sana.

Alianza soka yake ya kulipwa akichezea Uniao Sao Joao na mara akaitwa kwenye Timu ya Taifa ya Brazil akiwa na umri wa miaka 19, akawasaidia kufika fainali 1998 na kutwaa ubingwa wa dunia 2002.

Katika ngazi ya klabu, Carlos amecheza mechi 606 na licha ya kuwa beki amefunga mabao 75 katika miaka 21 aliyochezea gozi la ng’ombe. Akiwa na Real Madrid, Carlos alifunga mabao 46 katika mechi 370. Huyu ni mmoja kati ya wachezaji 19 tu waliopata kucheza zaidi ya mechi 100 za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ametajwa kama mmoja wa wachezaji mashuhuri 125 katika historia ya soka walio hai. Alistaafu soka Agosti 2012.

Pele:
Tumalize na mchawi wa soka, Edison Arantes do Nascimento, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Pele ambaye anarejewa na wengi kuwa ndiye mchezaji bora zaidi kupata kuzaliwa katika historia ya dunia na soka.

Alianza kwa jasho na damu, miiba na machozi kutokana na alivyozaliwa katika hali ngumu. Katika kuinusu familia nay eye mwenyewe kulala njaa, Pele alikuwa akifanya kazi kama mtumwa kwenye maduka ya chai. Alifundishwa kucheza soka na baba yake, lakini kutokana na umasikini alitumia soksi iliyojazwa matambara au magazeti chakavu.

Uvumilivu hulipa na alipanda hadi kuja kuwa katika kilele ambacho ni vigumu kusema kuna mwanasoka mwingine aliyefikia, na bao lake la kwanza lilikuwa dhidi ya Corinthians ambao walikuwa watani wa jadi wa klabu yake ya Santos.

Alicheza hapo mechi 605 na kufunga mabao yasiyomithilika 589. Baada ya misimu 17 hapo, Pele aliondoka na kujiunga na New York Cosmos mwaka 1975 alikofunga mabao 31 katika mechi 56.

Pele pia amefunga mabao 77 katika mechi 92 alizochezea timu ya taifa lake. Tangu kustaafu kwake 1977, amekuwa balozi mkubwa wa soka kote duniani na amekuza mchezo huu unaopendwa zaidi katika nchi mbalimbali. Amepata kuchaguliwa kama mwanamichezo wa karne, na uamuzi huo ulipitishwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki mwaka 1999. Pele kwa sasa ni marehemu.

*Imeandaliwa kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao.

Cio…

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button