Madaktari bingwa wafika Songwe huduma za kibingwa

SONGWE: TIMU ya madaktari bingwa na wabobezi 35 wanatarajia kutoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe.
Huduma hizo zitatolewa kwa siku saba katika hospitali za halmashauri zote za mkoani hapa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega amesema ujio wa madaktari hao mkoani hapa utawanufaisha wananchi kupata huduma hizo za kibingwa ambazo kuzipata kawaida ni ngumu kwao hasa wale wa vijijini.
SOMA ZAIDI: Madaktari Marekani watoa matibabu bure Moro
Amesema madaktari hao bingwa na bobezi 35 wametoka katika mikoa mbalimbali, ambapo wanategemewa kuhudumu kwa wa siku saba katika hospitali tano za Halmashauri za Mkoa wa Songwe.
Aidha, ujio wao ni sehemu ya mpango wa serikali kusogeza huduma za matibabu hasa ya kibingwa ambayo watu wengi wanahitaji lakini hawapati fursa hiyo.
SOMA ZAIDI: Madaktari bingwa kuwafikia watu 7,000 Arusha – HabariLeo
Daktar bingwa wa afya ya uzazi na magonjwa ya wanawake, John Lawi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ambaye pia ndie kiongozi wa timu ya madaktari bingwa waliokuja kwenye kambi ya Mama Samia Mkoa wa Songwe amesema lengo la ziara hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa ngazi ya Halmashauri zote tano za Songwe .
“Tutakaa Songwe kwa muda wa siku saba kuanzia mei, 26, mpaka 31, mwaka 2025 tunawaomba wananchi wa mkoa wa songwe kuitumia fursa hii kufika katika hospital zao za wilaya ili kupata huduma za kibingwa ambazo walikuwa wakisafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kupata huduma<” amesema Lawi.



