Machinga waagizwa kupisha njia maandalizi uzinduzi wa soko jipya

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wiki mbili kwa viongozi wa wafanyabiashara wadogo maarufu kama ‘Machinga’ waliopo Kariakoo kuhakikisha wanapisha njia za kuingia kwenye soko jipya, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na maandalizi ya uzinduzi rasmi wa soko hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 28, 2025 jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema ujenzi wa soko jipya la Kariakoo umekamilika kwa asilimia 98, hivyo ni muhimu maeneo ya njia kuu yakawa wazi ili kuwezesha shughuli za kibiashara kuanza kwa ufanisi.
“Tunapokwenda kuzindua soko hili, hatuwezi kuruhusu shughuli ziendelee kwenye barabara. Tunawapa wiki mbili viongozi wa Machinga kuhakikisha njia hizi zinafunguliwa,” amesema Chalamila.
Amesema kuwa wafanyabiashara wadogo watakaoondolewa katika maeneo hayo watapangiwa maeneo maalum ndani ya soko jipya, kwa mujibu wa maelekezo kutoka Wizara ya TAMISEMI, ambayo inatambua mchango wao kwenye uchumi wa eneo hilo.
SOMA ZAIDI: Chalamila: Ujenzi daraja Jangwani kuanza mwaka huu
Katika hatua nyingine, Chalamila amebainisha kuwa wafanyabiashara wote waliokuwa wakifanya kazi katika soko la awali kabla ya kuungua, na ambao walihakikiwa, watapewa nafasi zao upya.
Hata hivyo, watatakiwa kufuata utaratibu rasmi ikiwa ni pamoja na kujaza mikataba na kulipa kodi za maeneo watakayopangiwa.
“safari hi tumekwepa sana madalali ambapo kwa miaka mingi wamekuwa wakichukuwa vyumba vingi na kisha kukodisha kwa bei ya juu, hivyo sasa serikali itasimamia bei kuhakikisha wote watamudu, ”aliongeza.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Ashraf Abdulkarim, amesema shirika hilo linaendelea kuratibu urejeo wa wafanyabiashara waliokuwepo awali. Kati ya nafasi 1,520 zilizopo sokoni, wafanyabiashara 1,159 tayari wamejisajili na kukamilisha hatua za uhakiki kupitia mfumo wa TAUSI.
“Baadhi ya maeneo bado yapo wazi, hivyo tunakaribisha wafanyabiashara wenye nia ya kujiunga, ambao pia watafuata utaratibu rasmi kupitia mfumo huo,” amesema Abdulkarim.
Soko jipya la Kariakoo inalekea kuwa moja ya miradi mikubwa ya kisasa ya kibiashara jijini Dar es Salaam, likiwa na lengo la kukuza biashara, kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa ngazi mbalimbali, na kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia huduma na miundombinu ya kisasa.



