Chalamila: Ujenzi wa daraja Jangwani kuanza mwaka huu

DAR ES SALAAM; MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanza kwa ujenzi wa Daraja la Jangwani utakaoanza mwaka huu ili kuondokana na changamoto ya mafuriko iliyokuwa inawakumba wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Chalamila alieleza hayo juzi wakati wa mkutano wake na wanahabari uliofanyika mkoani humo.

“Kuhusu Daraja la Jangwani Rais (Samia) amedhamiria kwa dhati kwamba mwaka huu daraja hilo litaanza kujengwa na panapo majaliwa hakitakuja kuwa kilio kwa wakazi wa Dar es Salaam,” alisema.

Aliongeza: “Mkandarasi ameeshanza kujenga sehemu ya kuhifadhi vifaa vyake kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo… Waziri wa Ujenzi anaendelea na mikakati kuhakikisha mkandarasi anaanza kazi hiyo.”

Alisema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo serikali bado inaendelea na miradi ya ujenzi wa madaraja, barabara za lami na za kawaida, kuboresha vivuko na kuhamisha miundombinu ya maji na umeme ili kupisha ujenzi na utanuzi wa barabara.

Pia, Chalamila alieleza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umeomba bajeti ya Sh trilioni moja kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika bajeti itakayowasilishwa na Waziri wa Tamisemi, Mohamedi Mchengerwa wiki ijayo zitakazotumika kuboresha miundombinu ya afya, elimu na barabara mkoani humo.

Kuhusu uwekezaji katika bandari, Chalamila alisisitiza kuwa uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam imeongeza ufanisi mkubwa katika biashara baina ya Tanzania na nchi jirani na kuendelea kuifungua nchi.

“Tumeendelea kuona ufanisi mkubwa ndani ya bandari unaothibitishwa na wingi wa wageni wanaokuja kuchukua mizigo… hii inaonesha kuwa taifa limeendela kufunguliwa na mataifa yasiyo na bandari yameendelea kuiona Tanzania kama kivutio kwa sera zake imara za kibiashara.”

Amewaonya wanasiasa wanaokejeli uwekezaji huo akisema kwasasa ufanisi wa bandari umeongezeka kutokana na kuongezeka kwa maghala ya kuhifadhia mizigo inayopokelewa na bandari hiyo.

Katika hatua nyingine, Chalamila amewatakia heri ya Pasaka wakristo wote na wakazi wa Dar es Salaam kwa ujumla na kuwataka washerekee sikukuu hiyo kwa amani na utulivu akisisitiza polisi wapo kazini saa 24.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button