Uzinduzi wa mfuko kuleta fursa kilimo, biashara nishati safi

DAR ES SALAAM: Tanzania imepiga hatua muhimu katika juhudi za kukuza nishati jadidifu na maendeleo ya kilimo kupitia uzinduzi rasmi wa Mfuko wa PURE Growth Fund.
Mfuko huo unasimamiwa na Taasisi ya REEEP (Renewable Energy and Energy Efficiency Partnership) kwa ufadhili wa Serikali ya Austria.
Mradi huu mpya unalenga kuchochea mabadiliko katika sekta ya kilimo na nishati kwa kutoa EUR 2.5 milioni (zaidi ya Sh bilioni 7.6) kama ufadhili wa awali kwa Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) zinazojihusisha na nishati safi na kilimo.
Dirisha la kutuma maombi litakuwa wazi hadi 1 Agosti 2025, na utekelezaji wa miradi unatarajiwa kuanza Januari 2026.

Kwa mujibu wa Merja Laakso, Mkurugenzi wa Mipango wa REEEP, mpango huu utaondoa hatari kwa sekta binafsi, kuwezesha upatikanaji wa teknolojia, na kuunganisha huduma za nishati katika mnyororo mzima wa thamani ya kilimo – kutoka umwagiliaji hadi usindikaji na usafirishaji.
Kwa kusaidia teknolojia za nishati mbadala kushughulikia changamoto za uzalishaji na uhifadhi wa mazao, mfuko huu utaongeza uzalishaji wa chakula, kupunguza upotevu, na kuimarisha ustahimilivu wa wakulima dhidi ya changamoto za hali ya hewa.

Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Omary Mchengerwa, amesema:
“Uzinduzi huu ni hatua kubwa katika dhamira yetu ya kuimarisha maisha ya Watanzania kupitia suluhisho la pamoja kati ya nishati safi na kilimo.”
Kwa upande wake, Eva Kelly, Mkurugenzi Mtendaji wa REEEP, alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza kunufaika na mpango huu, na ni mwanzo wa jitihada pana zitakazofika nchi nyingine kusini mwa dunia.



