Mafanikio ya Tanzania EAC ni matunda ya sera madhubuti

TAARIFA ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, iliyowasilishwa bungeni kuhusu mafanikio ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ni ushahidi tosha wa dira sahihi ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha diplomasia ya uchumi na kukuza ushirikiano wa kikanda.
Takwimu zinazonesha ongezeko la miradi ya uwekezaji kutoka nchi wanachama wa EAC kutoka miradi 20 hadi 41 ndani ya mwaka mmoja ni ishara ya imani kubwa kwa Tanzania kama mahali salama na stahiki kwa uwekezaji.
Aidha, kupanda kwa thamani ya uwekezaji kutoka Dola za Marekani milioni 67.67 hadi milioni 133.44 ni mafanikio yanayopaswa kupongezwa kwa dhati.
Serikali imedhihirisha dhamira yake ya dhati si tu kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, bali pia kwa kuhakikisha kuwa vijana wa Kitanzania wananufaika moja kwa moja kwa kupewa ajira kupitia miradi hiyo.
Huu ni uthibitisho kuwa diplomasia ya uchumi inaendelea kuleta tija na matokeo chanya kwa wananchi.
Tunapongeza pia hatua za Tanzania kunufaika na soko la EAC kwa kuuza bidhaa mbalimbali za kilimo na viwandani.
Mafanikio haya yanajenga msingi imara wa uchumi shindani, unaojitegemea na unaoshirikiana kikamilifu katika mtangamano wa kikanda.
Hata hivyo, kama taifa, tunalo jukumu la kuendeleza kasi hii kwa kuhakikisha tunaimarisha zaidi uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa kimataifa, tukiwa na lengo la kuongeza ushindani katika soko la EAC na kwingineko.
Pia, tunashauri Wizara na taasisi husika kuendelea kuhamasisha sekta binafsi na wajasiriamali wadogo na wa kati kushiriki kikamilifu katika fursa hizi, huku wakipewa msaada wa kitaalamu na kifedha pale inapohitajika.
Kwa namna ya pekee, tunapongeza mchango wa Tanzania katika kipindi cha miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususani katika utekelezaji wa Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja.
Ufanisi huu unapaswa kuwa kichocheo cha kuongeza kasi ya maandalizi ya Umoja wa Fedha na Fungamano la Kisiasa ili Jumuiya iweze kufikia malengo yake kwa haraka na tija zaidi.
Kwa ujumla, mafanikio haya ni matokeo ya sera makini, uongozi thabiti na juhudi za pamoja kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi.
Tunahimiza kuendelezwa kwa ari hiyo katika kujenga uchumi shindani unaoweka mbele masilahi ya wananchi wake.



