Utandawazi, mila za kigeni zachangia ukatili nchini

KIGOMA: VIONGOZI wa dini na viongozi wa mila mkoani Kigoma wamesema kuwa jamii kuacha kuishi kwa kufuata misingi ya dini, mila na desturi za Mtanzania kumechangia kuendelea kwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na watoto mkoani hapa.
Viongozi hao wamesema hayo leo Mei 29, 2025 katika kikao kazi na viongozi wa dini, viongozi wa kimila, watu maarufu na wawakilishi wa vijana juu ya namna ya kuleta mabadiliko katika mila na desturi na kuondoa mila kandamizi kwa lengo la kupunguza ukatili wa kijinsia kilichoitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN WOMEN) kupitia mpango wa pamoja Kigoma (KJP).
Akizungumzia changamoto hiyo Mchungaji wa Kanisa EAGT Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Leonald Kibuguzo amesema kuwa nyumba za ibada zipo lakini wengi wao hawaishi kwenye mafundisho yanayotolewa kwenye nyumba hizo.

Viongozi wa dini, mila na vijana wakiwa katika kikao kazi cha kujadili juu ya namna ya kuleta mabadiliko katika mila na desturi na kuondoa mila kandamizi kwa lengo la kupunguza ukatili wa kijinsia
Mchungaji Kibuguzo amesema kuwa watu wengi kwa sasa wanaishi maisha yao kulingana na masuala ya utandawazi wanayoona watu wengine wanavyoishi kwenye nchi zilizoendelea na zinazoendelea ambapo hali hiyo inaleta changamoto kubwa kwenye malezi hapa nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa Kigoma, Mbonipa Bisama amesema kuwa maendeleo ya teknolojia yamekuwa yakitumika vibaya kutokana na watu wengi kuacha mila na desturi za Watanzania na kufuata mila, desturi na tamaduni za nje.

Azizi Nurfus Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma
Pamoja na viongozi dini kuwepo, viongozi wa mila na wazee kusema na kusisitiza jamii kufuata mila na desturi za watanzania kulingana na makabila na dini zetu viongozi hao wamesema kuwa miongozo hiyo imekuwa ikipuuzwa na idadi kubwa ya watu ambao wanafuata mipango na taratibu zao ambazo zinachangania ukatili.
Akifungua mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Azizi Nurfusi amesema kuwa viongozi wa dini na wazee wa mila na wazee maarufu kwenye jamii bado wanayo nafasi kubwa ya kuiasa jamii na jamii kuondokana na vitendo vya ukatili.

Mchungaji wa Kanisa EAGT Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Leonald Kibuguzo
Nurufus amesema kuwa kwa kutumia nafasi yao viongozi hao wanaweza kutoka na mkakati ambao utasaidia kuishauri serikali kutafuta namna bora ya jamii kuishi na kuondokana na changamoto za vitendo vya ukatili vinavyotokea kwenye jamii.



