Mwenge waweka jiwe la msingi miradi miwili Ilala

DAR ES SALAAM: MWENGE wa Uhuru 2025 umekagua na kuweka Jiwe la Msingi katika miradi miwili ya maendeleo kati ya saba iliyopo Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, na kuridhishwa na utekelezaji wake.

Miradi hiyo nishati safi ya gesi itokanayo na mafuta (LPG) katika Soko la Samaki Ferry, unaogharimu Sh milioni 216, ambao utanufaisha wakaanga samaki 48 pamoja na mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Magengeni–Chang’ombe–African School–Sanene yenye urefu wa kilomita 0.5, kwa gharama ya Sh miloni 678.

Akizungumza leo June3,2025 baada ya ukaguzi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Ismail Ali Ussi amesema miradi hiyo imetumia fedha nyingi za umma hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha inatunzwa.

“Niwaombe na kuwasihi wananchi kutumia vizuri miradi hii kwani imezingatia ubora. Tuwe mabalozi wa kuitunza kwa kutotupa taka katika mifereji, ili kuepuka kuziba mifumo ya maji na kusababisha maafa,”amesema Ussi.

Mwenge wa Uhuru una historia ya kuvutia

Akizungumzia mradi wa gesi, Ussi amesema unalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kusambaza nishati safi ya kupikia. “Kila mkaanga samaki atafungiwa mita yake na kulipia kulingana na matumizi. Hii itawasaidia kuepuka matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni hatari kwa afya na mazingira,” ameeleza.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alisema kuwa matumizi ya gesi badala ya kuni yamekuja kupunguza gharama za uendeshaji kwa wakaanga samaki, kuongeza kipato chao, na kuboresha mazingira ya kazi.

“Mradi huu pia utasaidia kuokoa misitu yetu inayokatwa kwa ajili ya kuni na mkaa. Ni mradi wa kimkakati unaotekelezwa kwa ushirikiano na Kampuni ya Oryx hivyo tuupokee na tuulinde ikutoa moyo wa kuletewa mingine mingi katika soko letu,” amesema Mpogolo.

Akizungumzia barabara ya Magengeni, Mpogolo ameongeza kuwa lengo kuu ni kupunguza msongamano wa magari katika maeneo ya Tabata Segerea, Barakuda, na Chang’ombe, jambo litakalorahisisha shughuli za uzalishaji.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala, Mhandisi John Chacha, amesema kuwa barabara hiyo inaunganisha mitaa yenye shughuli nyingi za kiuchumi na biashara katika Kata ya Liwiti.

“Mradi umeshakamilika kwa asilimia 70, na tayari Sh milioni 385 ambazo ni sawa na asilimia 52 ya bajeti zimekwishatumika. Pia, umetengeneza ajira kwa zaidi ya watu 50,” amesema Chacha.

Kwa upande wake,mmoja wa wakaanga samaki katika Soko la Ferry, Mwanahawa Juma amesema mradi huo umefika wakati mwafaka na ni mkombozi kwao kwani upatikanaji wa Kuni ulikuwa ni changamoto pamoja na bei yake kuwa juu ukilinganisha na gesi.

“Nishati ya gesi ni safi, haina moshi unaodhuru macho na mapafu. Itaboresha maisha yetu sokoni na hata majumbani,” amesema Mwanahawa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button