Mwenge wa Uhuru una historia ya kuvutia

DAR ES SALAAM; Mwenge wa Uhuru: Mwangaza wa Uhuru, Umoja, na Maendeleo ya Taifa la Tanzania.

KIla Desemba 9, Tanzania Bara  inasherehekea siku muhimu, siku ya uhuru, huku ikienzi moja ya alama kubwa za taifa letu, Mwenge wa Uhuru.

Mwenge wa Uhuru ni ishara ya nguvu, matumaini na mwangaza, mwangaza unaoongoza taifa letu kuelekea maendeleo, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Advertisement

Huu siyo tu Mwenge wa kawaida, bali ni alama ya hadithi ya harakati za Uhuru, maono ya Mwalimu Julius Nyerere, na safari ya Tanzania kutafuta amani na ustawi.

Hadithi ya Mwenge wa Uhuru inaanza kabla ya uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961, wakati ambapo aliyekua muongazaji wa harakati za Uhuru na Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema mbele ya baraza la kikoloni mwaka 1958 kwamba alikusudia kuwasha Mwenge wa Uhuru mara tu Tanganyika itakapopata uhuru.

Ahadi hiyo ya baba wa taifa  ilikuja kutimizwa baadae Desemba, 1961, wakati Tanganyika ilipopata Uhuru kutoka katika utawala wa kikoloni wa Mwingereza.

Baba wa Taifa alitimiza ahadi hiyo akiwa na matumaini ya kuona Tanganyika ikianza safari yake mpya ya kujenga taifa lenye amani, maendeleo, na umoja.

Mwenge wa Uhuru ulizinduliwa kama ishara ya taifa kuamka kutoka giza la ujinga, ugonjwa, na umasikini.

Haikuwa tu ishara ya Uhuru, bali pia ni alama ya kuondoa ubaguzi, ukosefu wa usawa, na migawanyiko ya kisiasa au kikabila.

Mwalimu Nyererea alikuwa akisema: “Tunawasha Mwenge na kuupeleka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili uangaze zaidi ya mipaka ya taifa letu; kuleta matumaini kwa wasio na matumaini, upendo katikati ya chuki, na heshima pale palipo na dharau.” Maneno ambayo yanaendelea kuwa miongozo ya taifa letu.

Safari ya Mwenge wa Uhuru siyo ya maadhimisho pekee. Kila mwaka, kutoka Machi hadi Oktoba, Mwenge huu huzunguka nchi nzima, ukipita katika wilaya zote za Tanzania.

Huu ni Mwenge unaoongoza mabadiliko, huku ukileta mwanga kwa miradi ya maendeleo inayofanyika katika kila kijiji, kila mji na kila wilaya.

Ni ishara ya juhudi za wananchi kuimarisha miundombinu, huduma za afya, elimu, na ustawi wa jamii.

Hatua hii, inayosimamiwa na Ofisi ya Rais, inajumuisha uteuzi wa viongozi wa mbio za Mwenge, na bajeti inayotengwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Mwenge unavua giza na kuleta mwangaza wa maendeleo kote nchini.

Mwenge wa Uhuru una historia ndefu ya maono, kwa sababu haujakuwa tu alama ya kumbukumbuku katika taifa letu.

Mwaka 1961, Brigedia Alexander Nyirenda, Ofisa wa Jeshi  alikamilisha dhamira ya baba wa taifa  kwa kuuweka Mwenge huo juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Safari hiyo ya kihistoria ilikuwa na watu 11, akiwemo Nyirenda, ambaye alitumia siku 16 kuhakikisha kuwa Mwenge wa Uhuru unafika kileleni kwa heshima na umuhimu mkubwa.

Mwenge wa Uhuru umejikita kwenye alama ya mwangaza wa kiakili, umoja, na umoja wa kitaifa.

Tangu wakati huo, Mwenge wa Uhuru umejizatiti kama ishara ya kudumu ya uhuru na matumaini, akionesha safari ya Tanzania kuelekea taifa lenye nguvu, lenye amani, na lenye mwelekeo wa maendeleo.

Katika kipindi hiki cha sherehe za uhuru, Mwenge wa Uhuru unawakumbusha Watanzania kuwa urithi wetu ni wa pamoja, na ni muhimu kuendelea kuthamini umoja wetu na juhudi za kila mmoja katika kujenga taifa.

Mwenge huu unaendelea kuwashangaza na kuhamasisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Unawakumbusha Watanzania kuwa tuna historia kubwa ya kushinda changamoto, na tuko pamoja kuhakikisha kwamba tunajenga Tanzania yenye usawa, amani, na ustawi kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Heri ya siku ya Uhuru kwa Watanzania……